Timu ya Simba Queens inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, kwa kufikisha alama 38, baada ya kuibanjua Young Princess mabao matano kwa moja Jana Ijumaa.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam ulishuhudia mabao ya Simba Queens yakifungwa na nahodha, Mwanahamisi Omary na Opa Clement kila mmoja alifunga magoli mawili huku lingine likiwekwa kimiani na kiungo wa kimataifa wa timu hiyo kutoka Burundi, Joelle Bukuru.

Bao la kufutia machozi la Yanga Princess katika mchezo huo wa mzunguko wa pili Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, lilifungwa na Shelder Boniface.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga Princess kubakiwa na alama 23 huku nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ambayo kila timu imecheza michezo 15 inashikiliwa na mabingwa watetezi, JKT Queens wenye alama 35 na Ruvuma Queens inafuata ikiwa na alama 34.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Simba Queens kuifunga Yanga Princess kwenye michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania bara msimu wa 2019/20. Mara ya kwanza Yanga Princess walikubali kufungwa mabao matano kwa sifuri Uwanja wa Karume, Dar es salaam.

Mtia nia Urais ACT - Wazalendo ameahidi kila mwananchi atafuga kuku 1000
DAS wa Handeni afariki kwenye ajali Dodoma, Mbunge ajeruhiwa