Tarehe 28, Septemba ya kila mwaka ni Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani na Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kichaa cha Mbwa: Chanja ili kukitokomeza”(rabies vaccinate to eliminate).

Kichaa cha Mbwa ni ugonjwa ulioathiri maeneo mbalimbali ya nchi yetu na maeneo mengine duniani, hususan bara la Asia na Afrika.

Ugonjwa huu unasababishwa na virusi jamii ya ‘lyssa’ ambavyo hukaa katika mate ya wanyama jamii ya mbwa walioathirika (mbwa, paka, mbweha, fisi na wengineo).

Binadamu hupata maambukizi pale anapoumwa na mnyama aliyeathirika, ambapo virusi huingia kupitia jeraha analopata na hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo.

Dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu, na baadaye ubongo, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa na mate mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimaye kupoteza maisha.

Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi na imani za kishirikina, hivyo hawaendi katika vituo vya kutolea huduma za afya, hutibiwa kienyeji hadi kupoteza maisha wakiwa nyumbani.

Takwimu zimekadiria kuwa ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa husababisha takribani vifo 59,000 kila mwaka duniani, ambapo kati ya vifo hivyo, asilimia 36 hutokea katika bara la Afrika ambapo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 hadi 50 ya waathirika wa kichaa cha mbwa ni watoto chini ya miaka kumi na tano, saabu wao ndio wanaokuwa karibu zaidi na mbwa (anayefugwa), na pia hupenda kucheza/kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani.

Ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba.

Pamoja na kusababisha vifo, ugonjwa huu unaleta athari kubwa katika uchumi kwani gharama ya chanjo kwa binadamu ni kubwa, takriban Tshs. 150,000/= kwa mgonjwa kwa bara la Afrika, ambayo ni sawa na asilimia sita ya mapato ya taifa katika bara hilo.

Kwa hapa Tanzania, ugonjwa wa kichaa cha mbwa uliripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo miaka ya 1932/33. Baada ya hapo, wagonjwa wameendelea kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa viwango tofauti.

Mwaka huu 2019, kuanzia mwezi Januari hadi Agosti, watu 16,290 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa na vifo nane (8) vimeripotiwa kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa na katika Halmashauri za Wilaya ya Ulanga na Malinyi watu 292 waliumwa na mbwa na kati yao wanne (4) walipoteza maisha.

Aprili mwaka 2018 tulipata mlipuko wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo watu sita (6) waliumwa na mbwa na kati yao watu wanne (4) walichelewa kwenda kupata chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa, hivyo waliugua na walipoteza maisha.

Utafiti uliofanyika mwaka 2002 nchini Tanzania ulibainisha kuwepo takriban vifo 1,499 kwa mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Katika kudhibiti tatizo hili, Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na Shirika la Chakula Duniani (FAO), walishirikiana na Dawati la Uratibu wa Afya moja, wakutoa chanjo 33,700 kwa ajili ya kufanya kampeni ya kuchanja mbwa.

 

Waziri amtaka Mkurugenzi kusitisha ujenzi wa kumbi za starehe Iringa
Video: Serikali yawaonya wanaobeza elimu ya watu wazima.