Kiungo kutoka nchini Ujerumani Emre Can amefanikisha dili la kusajiliwa moja kwa moja na klabu ya Borussia Dortmund, akitokea kwa mabingwa wa soka Italia Juventus siku 18 zilizopita.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, alitua Borussia Dortmund kwa mkopo mwezi uliopita, huku sehemu ya mkataba wake ukitoa nafasi kwa wababe hao wa Signal Iduna Park kumsajili moja kwa moja, endapo wataridhishwa na kiwango chake.

Alisajiliwa kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 21 sawa na Euro milioni 25, na tayari ameshaitumikia klabu ya Dortmund katika michezo mitatu, na kufunga bao moja.

Akiwa na mabingwa wa Italia, Can ambaye aliwahi kuwatumikia mabingwa wa Ulaya Liverpool kuanzia mwaka 2014–2018, alicheza michezo miwili ya Serie A, tangu The Bianconeri walipokua chini ya meneja Maurizio Sarri kuanzia msimu uliopita.

Alisajiliwa na Juventus akitokea Liverpool, akiwa mchezaji huru mwaka 2018, ambapo alicheza michezo 37 na kufunga mabao manne.

Kwa sasa Dortmund inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya Ujerumani (Bundesliga), ikiwa nyuma kwa alama nne dhidi ya vinara Bayern Munich.

Can aliwahi kucheza katika ligi ya Ujerumani akiwa na Bayern Munich (2011-2013) na Bayer Leverkusen (2013-2014).

Abiria waliokwama melini kwa kuvamiwa na Corona waanza kuokolewa
Atozwa faini laki 3 kwa kuua mke