Jumla ya shilingi milioni 600 zilizotengwa kwenye Mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya, Hamai kilichopo Wilayani Chemba Mkoani Dodoma zimeshindwa kutumika ipasavyo kufuatia Halmashauri kukosa wahandisi pamoja na kuchelewa kwa manunuzi ya vifaa vya ujezi na ufuatiliaji hafifu huku siasa zikichangia kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani humo, Dkt. Olden Ngassa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa changamoto kubwa imechangiwa na halmashauri kukosa wahandisi wa ujenzi kwa muda mrefu ambao ndio wasimamizi wakuu wa kazi za ujenzi pamoja na ushiriki mdogo wa wananchi uliosababishwa na upotoshaji wa kisiasa.

“kituo hiki kimecheleweshwa na mambo mengi na kusababisha kutumika kwa fedha nyingi licha ya majengo haya manne kufika katika hatua mbalimbali, changamoto hizo ni pamoja na kumalizika kwa fedha za ujenzi kutokana na ushiriki mdogo wa wananchi na kusababisha kutumika kwa fedha nyingi na hili limetokana na upotoshwaji wa kisiasa kwamba fedha zilizotolewa ni nyingi hivyo wananchi hawatakiwi kushiriki katika ujenzi, lakini sababu nyingine ni ukosefu wa rasilimali pamoja na usimamizi na ufuatiliaji,”amesema Dkt. Ngassa

Aidha, kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Ezekiel Odunga amesema kuwa ujenzi huo umeenda tofauti na maekekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo kwa kutotii maelekezo ya viongozi hali amabayo imepelekea kumfuta kazi afisa ununuzi vifaa pamoja na kuvunjwa kwa tiles ili kupitisha mabomba ya maji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amesema kuwa kushindwa kukamilika kwa wakati kwa kituo cha afya Hamai sio jambo zuri katika mkoa, hivyo ameagiza kukamilishwa mara moja kwa kituo hicho cha afya kwa Kutumia mfumo wa force account na jambo hilo halina mjadala

Nao baadhi ya wananchi kutoka Hamai baada ya kutajwa kuonyesha mwamko mdogo katika ujenzi wa kituo cha afya wamesema kuwa jambo hilo sio sahihi kwani wameshiriki kwa asilima kubwa.

 

Kada wa CCM Njombe akabidhi Miche 500 ya Parachichi
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 22, 2019