Moja kati ya mambo yaliyozua gumzo hasa wakati wa mashindano ya kombe la dunia ni picha zinazomuonesha mrembo ‘matata’ akiwa ndani ya mavazi ya ufukweni ambapo wengi waliaminishwa kuwa ni za Rais wa Croatia, Kolinda Grabar-Kitarovic. Lakini Dar24 inakushtua kuwa ilikuwa ndivyo sivyo.

Picha hizo ambazo zilianza kushika kasi kwenye Twitter, kiuhalisia ni picha za mrembo maarufu Coco Austin ambaye ni mke wa Rapa Ice-T, zilizopigwa na Paparazzi mwaka 2009 katika fukwe za Miami ambapo wanandoa hao walienda kustarehe.

Mkanganyiko wa picha hizo ulianzia Twitter baada ya mtumiaji mmoja wa mtandao huo wa kijamii alipoweka picha hizo za mrembo Coco mwenye umri wa miaka 36 na kuandika, “Croatian President, new crush alert.”

Ghafla ukawa mjadala wa utani kwenye mtandao huo ambapo watumiaji kadhaa walitania kuwa wanataka kwenda Croatia, wakiuliza namna ya kupita kwenye ubalozi wa Croatia ili wakutane na Rais Grabar-Kitarovic mwenye umri wa miaka 47.

Punde mitandao mahiri ya Afrika Kusini na Ufilipino iliichukua na kuiweka kama habari iliyozua gumzo. Mitandao hiyo pia kwa makosa iliweka picha za Coco Austin na kuonesha kuwa ni za Rais Grabar-Kitarovic, lakini baadaye waliandika habari ya kurekebisha makosa hayo.

Hata hivyo, habari hiyo ya kwanza iliendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, na hadi leo wengi wanaamini ni za rais huyo. Habari njema ni kwamba Dar24 imekushtua na hautakuwa mmoja kati ya walionasa kwenye mtego huo mbovu.

Grabar-Kitarovic, alikuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Croatia tangu mwaka 2015. Picha hizo za kuzushiwa zilimfanya kuwa maarufu katika kona nyingi za dunia.

Kwa bahati nzuri, Rais huyo pia hupenda kujichanganya na kufurahia upepo wa bahari akiwa na watu wa kawaida. Wakati wa Kombe la Dunia, alivumilia mvua na kuwapa nguvu wachezaji wa kikosi cha timu yake ya taifa kikishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Ufaransa (4-2) kwenye mechi ya Fainali nchini Urusi.

Habari kubwa katika magazeti ya leo Julai 29, 2018
Agundua jinsi ya kutumia SMS kubana matumizi ya umeme

Comments

comments