Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC ) limetakiwa kusikiliza ushauri wa wazawa kuhusu maeneo wanayoenda kusimika mitambo yao pale wanapofanya utafiti wa maeneo yatakayofaa kulingana na Jiografia ya eneo husika.

Ushauri huo umetolewa Wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza alipotembelea eneo lililowekwa mitambo ya TBC iliyopo katika eneo la Kwemashai kwa lengo la kutaka kubaini changamoto zinazosababisha kutokuwepo kwa usikivu kwa baadhi ya maeneo Wilayani humo.

“Changamoto kubwa katika Wilaya hii ya Lushoto ni Jiografia ya eneo hili kwani ina milima mingi sana kati maeneo yake yote hivyo ni vyema mkashirikiana na Halmashauri katika kuelekezana  eneo ambalo litakuwa na mlima mrefu zaidi kushinda yote ambao utawafaa kuweza kusimika mtambo wenu utakao rusha matangazo katika maeneo yote ya Wilaya hii,” amesema Shonza.

Shonza ameusisitiza uongozi wa TBC kanda ya Kaskazini kuhakikisha wanafanya utafiti huo haraka na kusimika mitambo hiyo mapema kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha inakamilisha usikivu kwa mikoa iliyoko karibu na maeneo ya mipakani kabla ya mwaka 2020 na ndiyo maana fedha za bajeti ya kuboresha usikivu zinatolewa kila mwaka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, January Lugangika alimuomba Naibu Waziri huyo kuzungumza na uongozi wa TBC kuweza kuwapatia mwandishi wa Wilaya hiyo ya Lushoto kwani kuhusu suala la ofisi tayari wamekwisha muandalia ipo.

Kwa upande wa Meneja wa Shirika la Utangazaji Taifa (TBC), Gerald Uisso amesema kuwa amepokea maelekezo yote na ofisi yake itahakikisha inazingatia ushauri na kufanikisha zoezi hilo la kuboresha usikivu mapema .

 

TANZIA: Mwanasiasa mkongwe nchini afariki dunia
LIVE: Kongamano la kumpongeza Rais Magufuli jijini Mbeya