Mamlaka ya Kupambana na Madawa ya Kulevya (DCEA) imethibitisha kuwa inamshikilia mfanyabiashara maarufu, Abdul Nsebo na mkewe Shamim Mwasha baada ya kuwakuta na madawa ya kulevya.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Oparesheni wa DCEA, Luteni Kanali Fredrick Milanzi, wawili hao walikutwa na dawa hizo aina ya heroine nyumbani kwao Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, Mei Mosi mwaka huu.

Ameeleza kuwa walifika nyumbani kwa wawili hao kwa kushtukiza baada ya kupewa taarifa ambapo walifanya upekuzi kwa muda wa saa sita kuanzia saa nane usiku hadi saa moja asubuhi.

Luteni Kanali Milanzi ameeleza walikuta dawa hizo ndani ya nyumba yao pamoja na nyingine ndani ya buti ya gari moja.

“Tulibaini dawa hizo zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba yao pamoja na kwenye buti ya gari, na uchunguzi wa awali uliofanywa na Mkemia Mkuu umebaini kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroine,” Luteni Kanali Milanzi ameiambia Mwananchi.

Ameongeza kuwa vitu vingine ambavyo wanavishikilia walivyovikuta nyumbani kwa wanandoa hao ni kadi za benki, simu tano, hati za kusafiria na nyaraka mbalimbali.

Aidha, ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa wao ni sehemu ya mtandao wa kimataifa wa biashara hiyo haramu wakiwa na washirika kutoka nchi mbalimbali duniani.

Amesema wanaendelea kuwashikilia kwa ajili ya upelelezi na kwamba upelelezi ukitimia watawafikisha mahakamani.

Chanzo: Mwananchi

Kikwete ataka habari za mtandaoni kifo cha Dkt. Mengi zipuuzwe, awataja wanaoujua ukweli
Watatu mbaroni kwa kukutwa na kobe 508