Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iko katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati wa Taifa wa miaka mitano wa kupanda na kutunza miti nchini.

Mpina ameyasema hayoleo Aprili 12, 2017 Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja mbalimbali Bungeni na kuongeza kuwa tatizo la uharibifu wa mazingira linamalizika.

Amesema kuwa Serikali inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 105 ambapo kila mwaka zitatengwa shilingi bilioni 20 kutoka vyanzo mbalimbali vya Serikali na wadau wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa mkakati huo.

“Taasisi za Serikali, Taasisi za madhehebu, Asasi zisizokuwa za Serikali,kambi za Majeshi, Magereza, Shule na makampuni kupanda na kutunza miti katika maeneo yao”,amesema Mpina.

Aidha,  Mpina amesema mkakati huo utasaidia kuokoa mazingira kwani mpango uko tofauti na mikakati mingine iliyopita kwani kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini itahakikisha kwamba miti inayopandwa inatunzwa na kukua.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitekeleza zoezi la upandaji miti kote nchini kupitia Ofisi hiyo ambapo kila Halmshauri inatakiwa kupanda miti 1,500,000 kila mwaka na kuhakikisha inatunzwa.

Mahakama yamfutia Gwajima kesi ya lugha ya matusi dhidi ya Kardinali Pengo
Video: Mbunge Kessy Adai Roma alimtukana Rais