Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imewatoa hofu wakulima wa mikoa ya kusini kuhusu uwezo wake wa kununua korosho zote na kuzihifadhi kabla ya kipindi cha mvua za masika.

Akizungumza wakati anahitimisha siku ya kwanza ya oparehseni ya ukaguzi wa maghala kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Joseph Buchwaishaija amewataka wakulima kuiamini Serikali kwakuwa ina uwezo wa kutosha wa kufanya zoezi hilo kwa muda na kwa ufanisi.

“Nachukua nafasi hii kuwatoa wasiwasi wakulima wote kwamba, maghala na sehemu za kuhifadhi korosho zetu sio tatizo tena, na tutahakikisha korosho zote zilizopo kwenye AMCOS (vyama vya msingi) tunazisafirisha haraka iwezekanavyo kabla ya msimu wa mvua kuanza,” amesema Prof. Buchwaishaija.

Aidha, ziara hiyo pia ilikuwa na lengo la kukutana na makumpuni ya kubangua korosho ambayo yameonesha nia na utayari wa kufanya kazi na Serikali wakati zoezi la ubanguaji litakapoanza.

Katika ziara hiyo Prof. Buchwaishaija pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Viwanda) Ludovick Nduhiye na maafisa wengine waandamizi wa wizara hiyo walifanikiwa kukagua maghala ya korosho kwenye wilaya za Mtwara, Mtama, Masasi na Nachingwea na kubaini kuwa maghala makuu na yale ya uhifadhi yana nafasi ya ziada kuhifadhi korosho zaidi ya tani elfu arobaini na nane.

Operesheni ya ukaguzi wa maghala mikoa ya kusni inatarajiwa kuendelea kwenye wilaya za mkoa wa Ruvuma kesho.

Video: Mbunge amsemea Nassari kwa JPM, Mrema amkingia kifua, 'Alikuwa anasoma'
Video: Maneke aanika ya wasanii aliowafanyia kazi bure wakavimba na mamilioni

Comments

comments