Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) imetoa kiasi cha Tsh. Milioni 700 kwa wabunifu 60 ili kuendeleza tafiti na bunifu zao na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.

Ameyasema hayo wakati wa Kongamano maalum la Ubunifu lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na COSTECH katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam (DITF), ambapo amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatambua wabunifu na wagunduzi wa kazi mbalimbali nchini.

Amesema kuwa kwasasa wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na bunifu za kazi mbalimbali lakini zimeshindwa kutambulika na hivyo kuilazimu Serikali kuanza kuweka utaratibu maalumu ikiwemo kuandaa mwongozo unaotarajiwa kuwatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali.

“Mwaka jana tuliandaa mashindano maalumu ya ubunifu na walipatikana washindi wa kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalumu wenye utaratibu wa kuendesha vituo vya teknolojia na ubunifu,”amesema Ole Nasha.

Aidha, Ole Nasha ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuandaa kongamano la kila mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na  wabunifu hao kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini kazi mbalimbali za wabunifu na watafiti na kuweza kutambulika.

Kwa mujibu wa Ole Nasha amesema wabunifu na wagunduzi nchini kutambua kuwa masuala ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na kuwataka wabunifu wasio katika sekta rasmi kuendelea kubuni bidhaa na vifaa mbalimbali kwa kuwa COSTECH si taasisi inayowagusa wasomi peke yao bali wabunifu wote waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Prof. James Mdoe amesema Serikali itaendelea kuzitambua kazi mbalimbali za wabunifu na wagunduzi nchini ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano madhubuti kwa ajili ya kutambua na  kuendeleza kazi za ubunifu na ugunduzi nchini.

Naye Mbunifu wa Maji taka kutoka Kampuni ya Biocon Africa Ltd, Prof. Karoli Njau ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wabunifu na wagunduzi wote nchini ili waweze kuonyesha kazi zao na kuhakikisha kuwa kuna utaratibu mzuri wa kuwapata watoa huduma katika kazi mbalimbali zinazoweza kupatikana nchini.

Balozi wa Uingereza nchini Marekani ajiuzulu
Wakulima wa Kilimo cha Umwagiliaji wapigwa msasa

Comments

comments