Vitendo vya baadhi ya Wanachi kukata miti ili kupata kuni za kupikia na utengenezaji wa mkaa, vimetajwa kuchangia mabadiliko ya tabia nchi na hivyo wahusika wametakiwa kuacha tabia hiyo mara moja na kushauriwa kutumia nishati mbadala, ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene, akiwa katika eneo la Pwaga lililopo wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma,  na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano juu ya suala hilo.

Amesema, wananchi wanatakiwa kuachana na tabia ya kukata miti kwa ajili ya kuni au mkaa na kuongeza kuwa vitendo hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa ukame na kwamba tabia hiyo ikiendelea nchi itakua katika tishio la kuwa jangwa.

Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe lililopo Wilayani Mpwapwa, amesema ni muda muafaka kwa wananchi kuanza kutumia nishati ya gesi katika shughuli mbalimbali zinazohitaji moto, na kusisitiza suala la upandaji miti katika maeneo athiriwa.

“Tunachezea uhai wetu kwa kuharibu mazingira, ukataji hovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa unamaliza miti kwa kiasi kikubwa, natahadharisha kuwa jambo hili halivumiliki na linahitaji ushirikiano kulikomesha,” Amesisitiza Simbachawene.

Awali akizungumza katika eneo hilo, Afisa Elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, Nelson Milanzi, amesisitiza juu ya suala la utunzaji wa mazingira, akitaka uwepo ushirikiano si tu kwa wadau wa mazingira, wananchi na Serikali, bali hata kwa wanafunzi pia.

“Naunga mkono juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla kutokana na ukemeaji wa jambo hili, ikiwemo upandaji wa miti kwa wingi na kuwachukulia hatua wanaohusika na uharibifu wa mazingira,” Amesema Millanzi. 

Juhudi za Serikali katika kukemea vitendo vya uharibifu wa mazingira, zimekuwa zikionekana katika maeneo mengi nchini, huku suala hilo pia likipigwa vita na Viongozi mbalimbali barani Afrika na Mataifa makubwa Ulimwenguni.

Wanawake Njombe wajipanga uchaguzi serikali za Mitaa
Watumishi wa Ardhi ‘waliokacha’ Mafia kikaangoni