Serikali imeingia Mkataba na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), kwa kusaini makubaliano ya awali ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi na Uzalishaji wa Mbegu Bora za Mazao ya Kilimo nchini.

Mkataba huo umesainiwa jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Uwekezaji Dorothy Mwaluko na Mkurugenzi wa IFAD kwa nchi za Tanzania na Rwanda Francesco Rispoli Oktoba 11, 2019.

Akiongea wakati wa utiaji wa saini mkataba huo Katibu Mkuu, Mwaluko amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ili kujiletea maendeleo kwa kuzingatia mchango wa sekta ya Uvuvi na Kilimo nchini.

“Makubaliano haya ya awali na Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo yana matarajio makubwa na ni mwanzo mzuri kwa maendeleo yetu katika nyanja za kilimo kwenye uzalishaji wa mbegu bora na uvuvi na ndio maana leo hii tumeusaini,” Mwaluko.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleleo ya Biashara kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Jackline Shayo ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kusema makubaliano hayo yataleta chachu katika kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi nchini kwa kuzingatia malengo kusudiwa.

“Naipongeza Serikali kwa hatua hii ya awali na  endapo Mfuko huu utatekeleza malengo kama ilivyokusudiwa itasaidia kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo kupitia uboreshwaji wa miundombinu ya uzalishaji wa mbegu bora,” amefafanua Bi. Shayo.

Mkataba huo wa awali uliosainiwa baina ya pande hizo mbili umelenga kuhakikisha kuna ongezeko la uzalishaji wa mbegu bora za mazao na samaki ili kuwepo na tija katika sekta ya Uvuvi na Kilimo nchini .

UWT yasisitiza madaraka 50 kwa 50
Chuo kikuu Moi chafungwa kwa vurugu za wanafunzi