Serikali imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa zinazotangazwa kupitia mitandao ya kijamii kutokana ubora wake kutothibitishwa na Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA).

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa wito huo Jijini Dodoma hii leo Oktoba 23, 2019 mara baada ya kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Amesema kumekuwa na wimbi la watu tofauti wanaotoa matangazo holela ya kuuza dawa za aina mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na kwamba hatua hiyo ni batili kwakua hazijathibitishwa na hazina baraka za TMDA.

“Kuuza dawa ambazo hazijazidhitishwa ni kosa kisheria na niwatake wahusika wanaotoa matangazo kuacha tabia hiyo mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao maana ni ukiukwaji wa wazi,” amesisitiza Waziri Ummy.

Aidha amesema dawa siyo bidhaa kama ilivyo bidhaa nyingine ambazo mtu anaweza kununua atakavyo kutokana na mahitaji au uwezo alionao na kwamba isipothibitishwa na mamlaka au daktari ni sumu inayoweza kugharimu maisha ya mtumiaji.

Waziri Ummy amesema tayari Wizara yake imeanza kuchukua hatua za kupambana na matangazo ya dawa na chakula mitandaoni bila kusajiliwa na kwamba tayari mtu mmoja amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kutangaza dawa ya kuongeza viungo vya wanaume na kwamba alimtuhumu yeye (Waziri Ummy) kufungua duka husika taarifa ambazo ni batili.

“Taratibu zipo wazi kama kuna watu wanaotaka kuuza dawa inawapasa kufuata utaratibu zilizowekwa kisheria kuepuka kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” amongeza.

Kikao hicho cha kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii kimepokea na kujadil taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka ya dawa bungeni jijini Dodoma.

Makocha 200 wakitaka kibarua cha Ndayiragije
Samia mgeni rasmi ufunguzi semina ya wabunge wanawake Jumuiya ya Madola