Serikali imesema kuwa imeweka nguvu kubwa na msisitizo katika kupambana na rushwa, kwani rushwa imekuwa ikirudisha nyuma juhudi za kupambana na umasikini, kujikomboa kiuchumi na kupoteza haki za watu wengi katika jamii.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damasi Ndumbaro wakati akizungumza kwenye kongamano la siku maalumu ya mapambano dhidi rushwa kwa nchi za umoja wa Afrika (AU).

Amesema kuwa kama nchi wameweka mkazo mkubwa kuhakikisha wanapambana na rushwa, na kwa kuhakikisha hayo yanafanikiwa Tanzania imejiunga na  kusaini mikataba na itifaki za kupambana na rushwa kimataifa na kikanda.

“Tanzania kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na rushwa imesaini na kuridhia mikataba na itifaki za kupambana na rushwa kimataifa na kikanda, hii ni pamoja na mikataba ya umoja wa kimataifa wa kupambana na rushwa,” amesema Dkt. Ndumbaro

Aidha, ametaja baadhi ya mikataba hiyo ni mkataba wa umoja wa mataifa wa kupambana na rushwa (UNCAC,2003), itifaki ya nchi za kusini mwa bara la Afrika ya kupambana na rushwa(SADC Protocol Against Corruption, 2001, na mkataba wa mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za afrika(AU Convention on preventing and Combating Corruption, 2003).

Nyingine ni mwanachama wa shirikisho la taasisi za mapambano dhidi ya rushwa barani  Afrika(AAACA) jumuiya ya madola(CAACA) pamoja na Afrika mashariki( EAAACA), ambapo amesema kuwa Tanzania pia ni mwenyeji wa bodi ya umoja Afrika ya ushauri kuhusu maswala ya rushwa ambapo makao makuu yake yapo Arusha.

Amesema kwa mkazo huo tafiti zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango  cha utawala bora kwa kupata asilimia 58.5/100.

“Tanzania imeonekana kuongeza kiwango cha utawala bora kwa kupata alama 58.5/100,na kuwa nchi ya kumi na moja11 kati ya nchi 54 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na 2017 ambapo ilipata alama 57.5/100 na kuwa nchi ya 17 katika bara la Afrika kwa mujibu wa Mo Ibrahim Index of African Governance” ameongeza

Aidha, amewataka TAKUKURU kuhakikisha wanafanya kazi kwa uwazi na waminifu ili kukomesha vitendo vya rushwa hapa nchini na kuwa na utawala bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP, Diwani Athumani amesema kuwa wao wamekuwa wakifanya kazi na kuhakikisha wanakomesha vitendo vya rushwa hapa nchini.

 

Mbunge wa Njombe Mjini ateta na Wajasiriamali
Mambo matatu muhimu yatajwa katika miaka mitano ya M-Pawa