Chama Cha Viziwi Nchini (CHAVITA) kimetakiwa kufanya ushawishi kwa serikali kupitia wizara ya elimu, ili kuwezesha somo la lugha ya alama kuingizwa katika mtaala wa shule na vyuo, kwa lengo la kufikisha elimu hiyo kwa watu wengi ili kurahisisha mawasiliano.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo wakati wa kufunga mafunzo ya lugha ya alama kwa wadau mbalimbali ikiwamo Polisi, Mahakama, Magereza na Uhamiaji, mwanasheria kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera, Jovin Ruttainulwa, amesema kuwa somo la lugha ya alama kuingizwa katika mtaala itasaidia kupatikana kwa watalaamu na wananchi wenye ufahamu wa lugha hiyo.

“Inaweza ikapangwa ianzie wapi, katika elimu ya msingi, sekondari au vyuo, lakini kwa upande wa pili maana huu ni utatuzi wa muda mrefu, kuna umuhimu mkubwa sana kwa Chavita kuwafikia watendaji wa mitaa, vijiji na kata, pia maafisa tarafa maana hawa ndiyo wanafanya kazi zao za kila siku karibu na wananchi,”amesema Ruttainulwa.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Uhamiaji Wilaya ya Bukoba, Wingi Momboka amesema kuwa, katika zoezi la uandikishaji vitambulisho vya taifa walikutana na changamoto ya kushindwa kuwasiliana na viziwi na kutoa mfano kuwa kuna sehemu walikwenda wakakuta familia nzima ni viziwi.

Naye, Ramadhani Masimbo mkaguzi msaidizi wa polisi upande wa idara ya usalama barabarani amesema kuwa Viziwi pia ni watumiaji wa barabara ambao nao wanakumbana na changamoto zilizoko barabarani ikiwamo kupata ajali na kuwa linapotokea hilo ni vigumu kuwasiliana nae.

Kwa upande wake mwezeshaji katika mafunzo hayo ambaye ni mwalimu wa elimu maalum kutoka shule ya sekondari Rugambwa iliyoko katika Manispaa ya Bukoba, Barnabas Matuta ameiomba serikali na watendaji wanaohusika kuyafanyia kazi mapendekezo wanayoyatoa ili kurahisha mawasiliano kati ya viziwi na makundi mengine.

Kwa mujibu wa mratibu wa mradi huo wa ushawishi na utetezi wa haki za viziwi, Judith Kashuliza,  Chavita walipata shilingi milioni 12.5 kutoka shirika la The Foundation For Civil Society kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya ushawishi kwa wadau mbalimbali.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 30/2019
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 30, 2019