Serikali imesema kuwa mabadiliko kwenye sekta ya sheria nchini hususani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yameanza kuleta tija baada ya kuongeza ufanisi na kuokoa fedha ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kuwalipa mawakili binafsi.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ambaye alitaka kujua kiasi cha fedha ambacho serikali imeokoa tangu maboresho kwenye sekta hiyo yaanze kutekelezwa.

Amesema kuwa kwenye Mwaka wa Fedha 2018/19 pekee Serikali imeweza kuokoa zadi ya shilingi bilioni tisa (9,018,957,011), ambazo kama sio maboresho kwenye sekta hiyo zingetumika kulipa makampuni binafsi ya uwakili.

Aidha, Dkt. Mahiga amesema kuwa Serikali itaendelea kutumia Mawakili binafsi kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali pale itakapothibitika kuwa ni lazima kufanya hivyo.

Ametoa mfano wa vigezo vinavyotumika kutumia mawakili binafsi ni shauri kufunguliwa kwenye mahakama ambazo sio za kimataifa na sheria za nchi husika haziruhusu uwakilishi wa mwanasheria kutoka nje ya nchi hiyo.

Kuhusu baadhi ya mashirika ya umma kuendelea kutumia mawakili binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amesema kuwa mashirika hayo ni yale ambayo mashauri yake yalianza kabla ya maboresho kwenye sekta hiyo hayajaanza kutekelezwa na uendeshaji wa mashauri utatekelezwa kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa Serikali.

Onyango azidi kuwa gumzo mitandaoni
Simba yadondosha kifaa kingine