Maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya urais ya mgombea wa Chadema chini ya mwanvuli wa Ukawa, Edward Lowassa yameanza na changamoto baada ya ombi la kutumia uwanja Mpya wa Taifa kutupiliwa mbali.

Lowassa na kambi ya Ukawa kwa ujumla walikuwa wanatarajia kufanya uzinduzi wa kampeni Agosti 22 mwaka huu katika uwanja huo mpya wenye muundo na sifa za viwango vya kimataifa ambao ulitarajiwa kutosha kubeba ‘mafuriko ya Lowassa’.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Bw. Assa Mwambene leo ameeleza kuwa serikali imekataa ombi la Chadema kumtaka mgombea wao kutumia uwanja huo kwa madai kuwa hawaruhusu uwanja wa serikali kutumiwa kisiasa na chama chochote.

Mwambene ameeleza kuwa idara hiyo ilipokea maombi ya Chadema Tarehe 12 Agosti na kwamba waliwajibu mapema kuwa ombi lao limekataliwa. Alieleza kuwa walishangaa kusikia na kuona taarifa zinazoeleza kuwa kampeni hizo zingezinduliwa katika uwanja huo wakati tayari walishatoa majibu kwa chama hicho.

Kambi ya Ukawa inatarajia kuzindua kampeni zake Agosti 22, siku moja kabla kambi ya CCM kufanya uzinduzi wa kampeni zake katika viwanja vya Zakhem Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Esther Bulaya Haepukiki Bunda, Wassira Kugawanya Nguvu
Chelsea Waipiku Man Utd Kumnasa Pedro