Serikali nchini imekiri kutokuwa na takwimu nyingi za magonjwa yasioambukizwa na hivyo kuzitaka taasisi mbalimbali za tafiti kuhakikisha zinawekeza kwenye mambo ya utafiti wa magonjwa hayo.

Aidha katika kukabiliana na magonjwa hayo pia Serikali inatarajia kufanya uzinduzi wa mpango huo ili kukabiliana na hali hiyo Novemba 14, 2019 Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Faustine Ndungulile wakati akifungua kongamano la kisayansi lililowakutanisha wadau wa sekta mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema kukosekana kwa takwimu nyingi za magonjwa yasiyoambukizwa imekuwa ni chanzo cha uwepo wa changamoto na hivyo kupelekea magonjwa hayo kuongezeka kwa kasi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

“Hakikisheni mnawekeza kwenye tafiti ili kuufanya mpango huu kufanikiwa maana tusipokuwa na takwimu za kutosha huu mpango hautakuwa na maana tafiti za kimfumo zinatakiwa ili tujue ni kwa nini tunakuwa na theluthi moja ya watoto wenye utapiamlo nchini wakati tuna chakula cha kutosha,” amesisitiza Dkt. Ndungulile.

Hata hivyo amesema ipo changamoto katika matibatu ya magonjwa hayo kwani mwananchi wa kawaida amekuwa akishindwa kumudu gharama na kutaka kuwepo kwa habari itakayosaidia kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na ushiriki wao katika utekelezaji wa mpango wa Serikali.

Awali Mkurugenzi wa tiba Wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe amesema tathimini ya hivi karibuni ya mpango mkakati wa sekta ya afya imegundua kuwa magonjwa yasiyoambukizwa yanachangia zaidi ya asilimia 30 ya vifo Kitaifa na asilimia 70 Kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Taifa ya utafiti wamagonjwa yabinadamu (NIMR), Yunus Mgaya amesema mzigo wa magojwa yasiyoambukiza ni mkubwa hali inayopelekea kuathiri maendeleo ya nchi kwani wanaosumbuliwa zaidi ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

“Tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanyika juu ya magonjwa yasioambukizwa na imebainika kuwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele yanachangia kuongezaka kwa vifo na mkutano huu utasaidia kuwa na kauli moja ya kuhakikisha tunapunguza magonjwa haya,” amesisitiza Mgaya.

Hata hivyo amebainisha kuwa utoaji wa elimu kwa jamii una mafanikio zaidi na kwamba kuna ulazima wa kuweka mikakati juu ya nini kifanyike ili kupunguza idadi ya wagonjwa na jinsi ya kupambana na kujikinga nayo.

Akiongea katika kongamano hilo mmoja wa vijana wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kisukari James Chumi amesema pia suala la imani za kishirikina zimekuwa zikichangia kwa watu wengi kuchelewa kufikishwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu.

Kutokana na hali hiyo Chumi ameiomba Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na uelewa wa magonjwa hayo kwani wengi huathirika kwa kukosa msaada wa mapema.

Sababu ya mama kumzika mwanaye akiwa hai
Watanzania mbioni kujipima Ukimwi kwa mate

Comments

comments