Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imefanya mapitio ya mwongozo yakinifu wa Umwagiliaji unaolenga kufanya mabadiliko na maboresho katika kilimo cha Umwagiliaji nchini.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Meneja msaidizi wa Mradi wa kujenga uwezo (TANCAID), Anthony Nyarubamba kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kikosi kazi wa kupitia mwongozo huo.

Amesema kuwa, mwongozo huo ambao ulikuwepo tangu mwaka 2010 ambao ulikuwa katika mfumo wa kitabu utaboreshwa na kuwekwa katika lugha rahisi na rafiki kwa watumiaji ambao ni wataalamu, wakulima na wadau wote katika sekta hiyo.

“Kabla ya kuwepo kwa Mwongozo huu wakulima wengi walikuwa wanadhani kuwa kilimo cha umwagiliaji ni kilimo chenye kutumia maji mengi lakini Mwongozo sasa utaonyesha matumizi sahihi ya maji sambamba na kujenga uwezo kwa wataalamu na wakulima nchini.” amesema Nyarubamba.

Aidha, amesema kuwa mtu yeyote atakayeshughulika na kilimo cha umwagiliaji nchini atatakiwa kufuata mwongozo huo ambao pia utachangia skimu za kilimo cha umwagiliaji nchini kujengwa katika ubora.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Ronald Komaga amesema kuwa tangu kuwepo kwa mwongozo huo mwaka 2010 kumejitokeza changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kitabu cha mwongozo huo kuwa kikubwa na siyo rafiki kwa watumiaji, mwongozo kutoeleweka kwa wadau wengi na baadhi ya vipengele kutotekelezeka.

Kikosi kazi hicho chenye kufanya mapitio na maboresho ya mwongozo huo wa kilimo cha umwagiliaji umehusisha washiriki kutoka Serikali za Mitaa, Ofisi za Kanda, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, na wawakilishi kutoka JICA.

Video: Mbwembwe za Piere akipanda ndege na Wabunge kwenda AFCON
Panado, konyagi vyatumika kupikia supu, hatari zake kiafya zatajwa