Serikali itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous kutokana na ukiukwaji wa taratibu zilizokuwa zimewekwa wa kuingia ndani ya  hifadhi hiyo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa juu ya hatua ambazo Serikali inazichukua kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria kuweza kuvua samaki.

“Mwaka 1994, wananchi wa Kata ya Mwaseni, Mloka, Ngoroka na Kipungila Wilaya ya Rufiji waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua Samaki. Hata hivyo, baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia ndani ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha sheria,” amesema Mhandisi Makani.

Aidha, amesema kuwa baadhi ya wavuvi wamebainika kujihusisha na vitendo vya ujangili wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa ajili ya kukausha samaki na kutengeneza mitumbwi pamoja na uharibifu wa mazingira unaotokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.

Mhandisi Makani amesema kuwa kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous.

Hata hivyo,amesema kuwa Wizara inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo jirani kutumia mabwawa mengine yaliyoko nje ya Pori hilo yenye fursa kubwa kwa kufanya shughuli za uvuvi.

 

Afrika kujiondoa mahakama ya ICC
#HapoKale