Serikali imekitaka Chuo cha Diplomasia kutoa taaluma ya vitendo kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho ili kuwawezesha wahitimu kuwa na mchango katika Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Akihutubia mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye ni Mgeni Rasmi katika mhafali hayo, amesema Serikali itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya stratejia, jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu hasa kwa muktadha wa kiafrika.

Waziri Kabudi ameongeza kuwa taaluma inayotolewa na Chuo hicho isiwe ya nadharia pekee bali iambatane na vitendo ili elimu hiyo itumike kusaidia kufafanua masuala ya Kidiplomasia na uhusiano wa Kimataifa yanayotokea duniani.

“Nakiagiza Chuo kuandaa mpango mkakati wa mafunzo kwa vitendo ili tuangalie ni jinsi gani Wizara inaweza kusaidia. Aidha, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama ilivyopendekezwa ili kisipitwe na wakati. Dunia inabadilika kwa kasi. Nasi hatuna budi kwenda kwa kasi hiyo,” Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ni vyema Chuo kikawa mstari wa mbele kutoa mafunzo hayo kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, na wafanyabiashara waliopo hapa nchini.

“Nimefarijika kusikia kuwa mmefanya mazungumzo na Chuo cha ISRI cha Angola kwa nia ya kufikia makubaliano ya kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili nchini Angola ambapo rasimu ya Hati ya Makubaliano imeandaliwa na inasubiri kusainiwa,” Amesema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi aliongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba Balozi za Iran, Libya, Urusi, Indonesia na China zimekuwa zikitumia wigo huu wa ushirikiano na kubadilishana uzoefu, kutoa mada mbalimbali chuoni hapo. Aidha, alitumia fursa hiyo kuzikaribisha ofisi nyingine za kibalozi hapa nchini kutembelea Chuo cha Diplomasia na kutoa uzoefu wao kwa vinafunzi pamoja na wakufunzi. Hivyo basi, ni vyema menejimenti ya Chuo kutoa mwaliko kwa Balozi zote na wawakilishi wa kudumu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuja kutoa uzoefu wao kwani nayo itakuwa sehemu ya diplomasia ya ulimwengu.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Drkt. Faraji Mnyepe amesema wahitimu 453 wametunikiwa vyeti baada ya kupata mafunzo na kufuzu ambapo kati yao 98 ni wa ngazi ya Astashahada ya Msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa Shahada, 83 ni wa Stashahada ya Uzamili, 45 Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.

“Nina imani kuwa wahitimu wa leo kama wale wa miaka ya iliyopita, wameiva ipasavyo katika fani za mahusiano ya kimataifa, Diplomasia na Stratejia. Naamin pia kuwa mtakuwa rasilimali kubwa kwa Taifa letu katika fani mlizosomea” Amesema Dkt. Mnyepe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe na Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi walifaulu vizuri masomo yao

Dkt. Mnyepe ameongeza kuwa, katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo kimeweza kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 1029 kwa 2018/19 hadi kufikia 1275 kwa mwaka wa masomo 2019/20 ambapo pamoja na mambo mengine juhudi zinaendelea katika kutanua wigo wa udahili kwa kuanziasha udahili wa mwezi Machi pamoja na kuanzisha program mpya.

“Katika mwaka wa masomo 2019/20 chuo pia kimeweza kupanua mawanda ya program zake kwa kuongeza idadi ya program za muda mrefu. Chuo kimeanzisha Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na Udhibiti wa Migogoro ambapo kwa sasa program hii inaendeshwa Dar es Salaam na Dodoma,” Amesema Dkt. Mnyepe.

Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi zetu mbili wa wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji. Kwa miaka yote hiyo, Chuo cha Diplomasia kimejikita kuwaandaa wanadiplomasia, wanastratejia na wabobezi wengi wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa.

Chuo kilitumika kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji na baadae kilipanua huduma zake na kutumika kuwaandaa pia wapigania uhuru wa nchi za Angola, Zimbabwe, Namibia n.k.

 

 

 

 

 

TBS yakanusha taarifa zinazosambaa kuhusu kinywaji cha ukwaju
Video: Twiga anawakilisha nini kwenye nembo ya taifa, sikiliza hapa majibu ya watu