Serikali Mkoani Simiyu imesema kuwa imeandaa mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwemo viwanda, kilimo na teknolojia, ambapo imejipanga kutoa ardhi bure kwa wawekezaji walio tayari kuwekeza mkoani humo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka katika ufunguzi wa kongamano la uwekezaji la Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali Waadiventista Wasabato (ATAPE), lililofanyika Mjini Bariadi Septemba 13, 2018.

Kiswaga amesema mkoa huo ni mkoa wenye ajenda ya maendeleo, hivyo umejipanga katika kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji katika fursa mbalimbali za uwekezaji mkoani humo.

“Mkoa wa Simiyu una fursa nyingi mkifika hapa chagueni tu sehemu mje kuwekeza, mtu atakayekuja kujenga kiwanda kikubwa, kizuri ardhi tutampa bure, sisi tutamuuliza tu kwamba tuandike jina gani kwenye hati na tutamkabidhi hati yake, kwa hiyo ATAPE pelekeni salamu kwa wawekezaji wenzenu kuwa ardhi ya uwekezeaji Simiyu ni bure, ninyi mtafute mtaji tu” amesema DC Kiswaga.

Ameongeza kuwa wawekezaji wote watakaowekeza mkoani Simiyu watapata soko la uhakika la bidhaa zao, huku akibainisha kuwa mkoa huo na mikoa inayouzunguka ina wakazi wasiopungua milioni 10 ambao watakuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zao watakazozalisha.

Hata hivyo DC Kiswaga ametoa wito kwa wawekezaji wote wakiwemo ambao ni wanachama wa  Chama cha Wanataaluma na Wajasiriamali  Waadiventista Wasabato (ATAPE), kuwekeza katika ujenzi wa hoteli na hosteli katika eneo la Nyakabindi mahali ulipo uwanja wa Nanenane Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

Watabiri wa hali ya hewa waonya kuhusu kimbunga Florence
Bondia Mwakinyo asepa na Milioni 7 Bungeni leo