Serikali imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo (mbegu, mbolea, viuatilifu na zana za kilimo) zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu.

Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ndanda, Cecil David Mwambe aliyetaka kufahamu kwanini Pembejeo za kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata mavuno haba na kama Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za madawa, mbolea na zana za kilimo.

Amesema kuwa Serikali ina utaratibu wa kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia Mfumo wa Ununuzi wa pamoja nchini kwa mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea, utaratibu huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu.

Aidha, ameongeza kuwa katika jitihada za kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima, Serikali hununua  na kusimamia uthibiti na usambazaji wa viuatilifu vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, Panya, Nzige wekundu na Nzi wa matunda.

Pia amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa mikopo nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.

Kwa upande wa mbegu na viuatilifu, Mgumba amesema kuwa serikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambao utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi.

Diamond afunguka kisa kuwatelekeza watoto wake Afrika Kusini, "Mwenzangu hataki"
Video: Mambo ya msingi ziara ya Rais Magufuli nchini Malawi