Leo Aprili 23, 2018 Bungeni jijini Dodoma kwenye kikao cha 15 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr Faustine Ndugulile, amesema Serikali imepanga kuanza kuwafuata watu katika maeneo ya mkusanyiko ikiwemo baa ili kuwapima magonjwa ya Ukimwi na Kifua kikuu (TB) hususani Wanaume hivyo watu wasishangae watakapoona utaratibu huo ukifanyika.

Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge Masoud Abdallah aliyetaka kufahamu serikali ina mikakati gani katika kutoa elimu maalum ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi zaidi.

“Serikali baada ya kuona kumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wakiathirika na ugonjwa wa TB na UKIMWI. Hivyo tumeamua kujielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari lakini vilevile tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi sambamba na hilo tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa TB na UKIMWI”, amesema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Ndugulile amesema kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumuweka katika matibabu ndio njia kuu ya kupambana na kulishinda tatizo la kifua kikuu jambo ambalo lipo kwenye mikakati ya serikali katika kufufua uwezo wa kufikia watu wote wanaohitaji huduma za TB ili kuwagundua mapema na kuwatibu kikamilifu.

Museveni aonya matumizi ya mdomo katika mapenzi
Jacob Zuma atangaza ndoa kwa mara ya 7