Serikali imewaonya watu wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwenye sekta ya Bima ya Afya nchini ikieleza kuwa mkono wa sheria hautawaacha salama.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Makampuni ya Bima ya Afya Tanzania (ATI), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile alisema kuwa Serikali inatambua kuwa udanganyifu huo hufanywa na baadhi ya watoa huduma za afya na watu wanaotibiwa kwa mfumo huo. Aliongeza kuwa wakati mwingine vitendo hivyo hufanywa kwa ushirikiano kati ya wafanyakazi wasio waaminifu pamoja na wateja.

Dkt. Ndugulile alitoa onyo kwa wanaojihusisha na udanganyifu kwa lengo la kuhujumu huduma za Bima ya Afya, kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo jela pamoja na faini.

“Serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapinga kwa vitendo rushwa na udanganyifu; na yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo huchukuliwa hatua kali za kisheria. Serikali hii imeelekeza nguvu zake katika kujenga mfumo na taifa lenye uadilifu,” alisema.

Alitoa wito kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa sekta ya afya kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya udanganyifu kwa vyombo husika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inathamini mchango wa makampuni ya bima ya afya nchini na kwamba inaendelea kuhakikisha kuwa kuna mazingira rafiki ya ushirikiano kati sekta binafsi na sekta ya umma, ili kuhuisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa bei nafuu kwa kila Mtanzania.

Aliongeza kuwa ingawa kiwango cha watu wanaojiunga na huduma ya afya nchini kinaongezeka ikiwa hadi sasa ni asilimia 32 tu ya Watanzania wote ndio waliojiunga na mfumo wa Bima ya Afya, na wengi wao ni wanaoishi mijini; kiwango hicho hakiridhishi kulingana na Malengo ya Afya kwa Wote ya kufikia asilimia 70 ya Watanzania ifikapo mwaka 2020.

Alisema ili kuhakikisha kuwa lengo hilo linatimia, pamoja na kutoa elimu na uhamasishaji, Serikali iko kwenye mchakato wa kuandaa muswada wa sheria itakayomtaka kila Mtanzania kuwa na bima ya afya na kwamba anaamini mwaka kesho inaweza kupitishwa na Bunge.

“Nitumie fursa hii pia kuwahamasisha wananchi wote kuwekeza katika bima ya afya kwa kujiunga na mifuko ya bima ya afya, kwasababu hakuna jambo muhimu kwa ustawi wa jamii kama kuwa na uhakika wa kupata huduma stahiki za matibabu wakati wowote,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa ATI, Suleiman Khamis aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma bora ya bima afya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile katika picha ya pamoja na wakuu wa taasisi binafsi za bima ya afya, kwenye mkutano wa wadau wa Bima ya Afya nchini uliofanyika leo katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam

Alisema kuwa majadiliano katika mkutano huo uliowahusisha wadau wa sekta binafsi na umma umehuisha utatuzi wa changamoto ya udanganyifu utakaoweka mfumo bora wa utoaji taarifa; pamoja na kujadili namna ya kuwa na bei elekezi itakayoweka viwango sawia vya gharama ya huduma ya bima afya.

Naye Elia Kajiba, aliyemuwakilisha Kamishna wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware aliwataka wadau wa sekta ya bima nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Bima ya Mwaka 2009.

Alisema kuwa Mamkala hiyo inaendelea kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya usimamizi wa sheria na inachukua hatua kali kwa wanaoenda kinyume na sheria kwani ukosefu wa uadilifu ni tishio la ustawi wa Taifa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau wa sekta ya afya ikiwa ni pamoja na wakuu wa taa, sisi za umma na binafsi zinazotoa huduma ya afya, makampuni ya bima ya afya pamoja na wawakilishi wa Wizara mbalimbali.

Fastjet yapewa notisi ya siku 28, yatakiwa ijitafakari
Rais Magufuli hajakosea kuniteua- Msekwa