Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na kampuni za simu ili kuwasaidia wananchi katika mambo mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya Afya, Elimu na Miundombinu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Tamisemi, Joseph Kandege katika hafla ya uzinduzi wa Vodacom Tanzania Foundation ambapo amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ili kuwawezesha Vodacom kuwafikia Watanzania wote wenye mahitaji .

Amesema kuwa Vodacom wanafanya kazi ambazo zinagusa jamii kama afya na kuwasaidia watoto wa kike kwenda shule kwa kuwapatia taulo za kujihifadhia wakati wa hedhi, pia wameendelea kuwasaidia kina mama juu ya ugonjwa wa Fistula ambayo inawapelekea wakina mama wengi kutengwa na jamii.

“Serikali itahakikisha inaimarisha miundombinu ili kuhakikisha Vodacom inawafikia watu wenye uhitaji na pia tumeona jinsi walivyoweza kuwasaidia watoto wa kike na wakinamama wenye Fistula juu ya kupata matibabu ya ugonjwa huo na kugawa vitaulo kwa watoto wa kike wenye uhitaji, ambao wanakosa kwenda shuleni pindi wawapo kwenye hedhi,”amesema Kandege

Aidha, ameongeza kuwa matarajio yake ni kuwa kazi inayofanywa na Vodacom iweze kufanywa na mashirika mengine kwa kushiriki jambo kama hilo au kwa kujiunga pamoja na Vodacom kufanya jambo hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation na Afisa Uhusiano, Rosalynn Mwaria amesema kuwa wamekuja kuonyesha matokeo chanya ya kazi walizokuwa wakizifanya kuanzia mwaka 2014 hadi 2017, wakiambatana na sekta binafsi pamoja serikali kwa kuwasaidia watoto na kinamama kwenye mambo mbalimbali .

Kwa mwaka 2019 hadi 2021, Mkurugenzi huyo amesema wamejikita katika miradi ya watoto katika Elimu na pia kufanya maendeleo ambayo yatawasaidia kutunza mazingira ya Tanzania nzima.

 

Bashe ang'aka, 'Hili genge la wahuni ipo siku nitawataja kwa majina'
Mjue zaidi mchezaji Krepin Diatta wa Senegal