Serikali imedhamiria kuendelea kujenga mazingira wezeshi na endelevu katika Sekta ya Kilimo kupitia sera imara na zenye kutekelezeka.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki wakati akifungua Kongamano la Tano la Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhusu Sera kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Amesema kuwa dhamira ya Serikali inaenda sambamba na mchango wa sekta ya Kilimo katika uzalishaji pamoja na ukuaji wa uchumi nchini kwa kuzingatia namna sekta hiyo inavyochangia katika maeneo mengi ikiwemo, utoaji wa ajira kwa wananchi waliowengi.

“Ni mambo ambayo yanajieleza yenyewe na kila mmoja wetu anayajua vizuri.  asilimia 65.5 ya Watanzania wanategemea ajira na maisha yao kwenye kilimo, pia kinachangia asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini na asilimia 65 ya mali ghafi ya viwanda vyetu,”amesema Kairuki

Aidha, amesema kuwa asilimia 30 ya fedha za kigeni hutokana na mauzo ya nje ya mazao na bidhaa za kilimo na huchangia asilimia 25 kwenye pato la Taifa.

Pamoja na jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta hiyo, Waziri amebainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo na sehemu kubwa ya kilimo kutegemea jembe la mkono, matumizi madogo ya mbegu bora zinazotoa mazao mengi na kuhimili maradhi na athari za kimazingira, matumizi ya maji ni kidogo pamoja na kilimo kutegemea mvua bila kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji chenye uhakika.

Kwa upande wake Naibu Waziri Kilimo, Omari Mgumba amesema kuwa jitihada za serikali kuendelea kuhakiki madai ya madeni yenye ukakasi ya Wakala wa pembejeo wanaosambaza mbegu na mbolea wanaidai serikali kiasi cha shilingi bilioni 35.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Chuo cha Kilimo cha Sokoine, Jackline Mkindi amepongeza uwepo wa kongamano hilo ambalo litatoa fursa za kujadili na kueleza changamoto wanazokumbana nazo hususani upande wa usambazaji wa Pembejeo nchini na madeni yaliyopo ambayo hadi sasa ni sh. bilioni 39.9 ambazo zinapaswa kulipwa na serikali.

Kongamano limeandaliwa na Jukwaa la Uchambuzi wa Sera za kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta binafsi na za umma ili kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo na kuchangia katika ukuaji wa Viwanda na kuhudhuriwa na takribani zaidi ya washiriki 300 nchini.

Video ya mwanamke anayejinyoa vinyweleo kwenye ‘bodaboda’ yatikisa
50 Cent achoma nguo za Gucci kupinga ubaguzi wa rangi