Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha mifumo yake ya utoaji huduma za dawa kutokana na ukweli kwamba dawa zinatumika kwa wanyama na binadamu na kuleta usugu wa ugonjwa husika kwa mgonjwa na gharama kubwa kwa taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa Ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa siku nne wa Jukwaa la kudhibiti usambazaji na uzalishaji wa bidhaa za madawa Afrika ambapo nchi 18 zinashiriki.

“Tanzania ni moja ya nchini iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika udhibiti wa dawa feki kwa Afrika nzima na mamlaka ya dawa na vipodozi nchini ina maabara za kisasa na watalaamu wa kutosha wa kuweza kufanya ukaguzi wenye ubora na viwango vya kimataifa,” amesema Ndungulile.

Ameongeza kuwa Tanzania imeweza kujitosheleza kwa dawa za kutosha na zenye viwango vya kimataifa na changamoto kubwa ilikuwa  kudhibiti dawa zinazoingia kwa njia ya panya ambapo tayari mamlaka husika wameshafungua ofisi za kanda ambazo zimefanya kazi kubwa kupunguza mianya ya dawa zinazoingia kwa njia ya panya.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Agnes Kijo amefafanua kuwa wataalamu kutoka nchi za Cameron, Ivori Coasti, Mali, Nigeria, Ghana, Burkina Faso, Mauritius, Senegal, Ethiopia, Sudan, Guinea, Sierra Leone, Uganda, Malawi, Zambia, Zimbabwe na Afrika kusini watakutana kwa siku nne ili kuja na mpango kabambe wa kudhibiti dawa bandia.

“katika mkutano huu jambo kuu litakuwa na kwa namna ngani tunaweza kudhibiti dawa bandia kwenye masoko na kuhakikisha kwamba wazalishaji pia wanatoa dawa zenye ubora unaokubalika katika soko,”
amesema  Kijo.

 

Video: IGP Sirro asisitiza nidhamu ya kazi
China kujenga Chuo cha usafirishaji nchini