Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewataka wafanyabiashara kujitokeza katika mnada wa hadhara wa meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.
 
Mnada huo unatarajiwa kufanyika Januari 29, 2018 Jijini Dar es salaam Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
 
Aidha, katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dkt. James Wakibara imesema kuwa mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.
 
Amesema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na 26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni kabla ya siku ya mnada huo.
 
Vile vile ameongeza kuwa wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.
 
  • Mpina akitwanga faini kiwanda cha Sanflag
  • Majaliwa: Hakikisheni mnatokomeza uvuvi haramu
  • Wananchi kushuhudia chimbuko la binadamu
 
“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” ameonya Mkurugenzi huyo

Ligi ya wanawake ya Serengeti Premier Lite kuendelea Februari
Jaji Mkuu atoa angalizo kwa viongozi na wanasiasa