Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kulijengea uwezo Bunge ili liweze kuisaidia Serikali kuleta maendeleo na kupunguza umaskini.

Majaliwa amesema hayo leo Septemba 14, 2017 wakati akizungumza na wabunge na Mawaziri katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa kulijengea uwezo Bunge (Legislative Support Project II –LSP II) kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

“Serikali inatambua umuhimu wa kushirikiana na Bunge, ikiwa ni pamoja na kuendelea kulijengea uwezo Bunge ili liweze kuisaidia Serikali kuleta maendeleo na kupunguza umaskini. Pamoja na changamoto zilizopo, tutaendelea kushirikiana na Bunge kuhakikisha kuwa ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili nchi yetu unapatikana,” alisema.

Amesema anaamini kwamba mradi huo utakuwa kichocheo cha kuimarisha zaidi uwezo wa Bunge na Kamati zake.

“Ni matarajio yangu, mradi huu utaimarisha zaidi uwezo wa Bunge na Kamati za Bunge kuchambua miswada ya sheria, kuishauri Serikali kusimamia mapato na matumizi, kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhakikisha masuala ya jinsia na mahitaji ya makundi maalumu yanahusishwa kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya Bunge,” alisema.

Pia Majaliwa amezishukuru nchi wahisani na washirika wa maendeleo ambao wanashirikiana na Bunge kutekeleza mradi huo. Wahisani hao ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Serikali ya Ireland, Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo la DFID, Serikali ya Denmark na Serikali ya Sweden.

Awali, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila wakati akitoa maelezo juu ya mradi huo, amesema uwepo wa mradi huo ni matokeo ya ushirikiano baina ya Bunge na UNDP ambao ulianza mwaka 2005. Mradi huo ulijulikana kama Uimarishaji wa Demokrasia (Deepening Democracy).

“Awamu ya kwanza ya mradi huu ilianza mwaka 2010 hadi 2016, na awamu ya pili inaanza mwaka 2017 hadi 2021 na mradi huo utagharimu dola za Marekani 12,765,600.00 lakini katika awamu ya kwanza tumepatiwa dola za Marekani milioni tatu”.

Amesema utekelezaji wa mradi huo, utalijengea Bunge uwezo katika masuala ya utungaji sheria, usimamizi wa bajeti za Serikali, ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za Bunge na usimamizi wa shughuli za Serikali kwa ujumla.

Naye Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Bodi ya Mradi huo, alisema ana matarajio kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wabunge waweze kuishauri Serikali kusimamia rasilmali za nchi.

Aliwasisitiza wabunge wakisikia mafunzo ya LSP II yanatolewa, wafuatilie kwa ukaribu na wajitokeze kwa wingi kushiriki mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa mradi huo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, David Omozuafoh, alisema uchaguzi wa mwaka 2015 uliwezesha Tanzania kupata idadi kubwa ya wabunge lakini hapakuwa na uwekezaji wowote kwenye sekretarieti ya Bunge.

Amesema Jumuiya ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa (UN WOMEN), itakuwa na jukumu la kusimamia masuala ya jinsia ndani ya Bunge kwa kushirikiana na Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG).

 

Korea Kaskazini yatishia kuigeuza Marekani kuwa mavumbi, kuizamisha Japan
Kubenea augua ghafla Dodoma