Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amesema kuwa serikali itaanza kusajili nyaraka na hati milki za ardhi ndani ya mkoa husika, badala ya utaratibu wa mwanzo wa kusajiliwa ndani ya kanda zilizokuwa zimetengwa lengo ni kupunguza ucheleweshaji wa usajili wa nyaraka hizo na kuepusha usumbufu wa wananchi.

Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua, mkutano wa wataalamu wa sekta ya ardhi na wakurugenzi na makatibu tawala wa mikoa, wanaokutana jijini humo, kutathmini malengo ya sekta hiyo, sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu hao namna bora ya ufanyaji kazi na namna ya kutatua changamoto zilizopo.

Amesema kuwa wamekusudia kuhamisha ofisi za kusajili nyaraka za ardhi kutoka katika kanda, na kuzirudisha ndani ya mikoa husika, ili kurahisisha zoezi hilo, na upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati, na tayari wakuu wa mikoa wameridhia na kutoa majengo yatakayotumika kama ofisi za wizara za usajili ndani ya mikoa.

“Nataka hatimiliki zote zitolewe na kusajiliwa mikoani kwani watu wamekuwa wakipoteza muda na gharama nyingi za usafiri kufuatilia hati hivyo hatuwatendei haki hawa wananchi wanyonge kwa kuwatwisha mzigo wa gharama,”amesema Lukuvi.

Aidha, amesema kuwa yupo mbioni kuandaa kanzi data ya matapeli wa ardhi na kuiweka katika tuvuti ya wizara ya ardhi ili wananchi wawajue na kujiepusha nao ili wasitapeliwe ardhi zao na watu hao na hata muogopa mtu yeyote.

Waziri Lukuvi pia amesema kuwa haitakuwa na maana kwa serikali kama itaendelea kuwapa mzigo wa gharama wanachi wake wakati wa ufuatiliaji wa hati miliki za maeneo yao na ndio maana wakaja na mpango huo.

“Tunataka kuwasaidia wananchi kupata hati miliki za maeneo yao huku gharama wanazozitumia ni nyingi leo hii unakuta mtu anatoka Kigoma anakuja Tabora, kufuata hati lakini tofauti na nauli anatumia siku saba hadi kumi kukamilisha zoezi hilo,”ameongeza Lukuvi

Mbali na hilo amewaonya watumishi wa idara za ardhi nchini kuacha tabia ya kupandisha bei ya maeneo pamoja na gharama za upimaji kwa madai kuwa wanajiongezea mapato ya ndani.

 

Kim Kardashian atinga Ikulu ya Marekani kumtetea Rapa Asap Rocky
Waziri Mkuu acharuka, aagiza wezi wa nondo wakamatwe