Gwiji wa mchezo wa Tennis duniani, Serena Williams amerejea rasmi ulingoni baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani miezi mitano baada ya kujifungua.

Akirejea upya na kwa kishindo, Serena aliungana na dada yake Venus Williams wakiunda Timu ya Marekani katika mchezo wa wawili wawili kwenye Michuano ya Fed Cup inayoendelea katika Jimbo la North Carolina.

Katika mchezo huo, ndugu hao wawili walijikuta wakichezea kichapo cha seti 6-2, 6-3 kutoka kwa Timu ya Uholanzi, lakini matokeo hayo hayakuwaumiza sana mashabiki wa mchezo huo nchini Marekani kwani habari kubwa ilikuwa ni kurejea kwake kwenye mchezo huo, huku akionesha kiwango cha hali ya juu.

Miongoni mwa mashabiki waliokuwa jukwaani wakimshangilia Serena, ni binti yake Alexis Olympia Ohanian Jr, ambapo baada ya mchezo Serena alieleza furaha yake kwa mwanaye kumshudia kwa mara ya kwanza akicheza tennis.

“Huu ni mchezo wake wa kwanza kunishuhudia nikicheza, nafurahi amepata fursa hiyo”, alisema Serena,

Huu ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimashindano tangu acheze kwa mara ya mwisho Januari mwaka 2017 alipotwaa taji la Australian Open akiwa na ujauzito wa miezi minane.

Serena mwenye umri wa miaka 36 alikuwa ameamua kutorejea kwenye mashindano yoyote mwaka huu, huku akiikosa michuano ya Australian Open ya mwaka huu kwa madai kuwa daktari wake alimshauri apumzike kwa muda usiopungua wiki sita.

Licha ya sasa kurejea ulingoni, bado hajaamua kama atashiriki katika mbio za kuwania mataji matatu makubwa ya Grand Slam yaliyobakia mwaka huu ambayo ni French Open, Wimbledon na US Upen.

JPM afanya uteuzi, apandisha vyeo maafisa wa JWTZ
Madudu ya Trump yaendelea kuibuliwa