Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy amezungumzia tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi kwa lengo la kumsaidia  katika uchaguzi wa urais mwaka 2007.

Sarkozy ambaye ameendelea kuhojiwa na kuchunguzwa na vyombo vya usalama nchini humo kuhusu sakata hilo, amesema kuwa ameundiwa sakata hilo kutokana na uamuzi wake wa kujihusisha na oparesheni ya majeshi ya NATO yakiongozwa na Marekani kumuondoa madarakani Gadaffi mwaka 2011.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63 amekaririwa na gazeti la Le Figaro akieleza kuwa tangu sakata hilo lilipoibuliwa amekuwa akiishi kama yuko kuzimu.

“Ninatuhumiwa bila ushahidi wowote. Ninaishi kama niko kuzimu kutokana na sakata hili la kunichafua tangu Machi 11 mwaka 2011,” amesema Sarkozy.

Serikali ya Ufaransa imemfungulia rasmi mashtaka kuhusu sakata hilo baada ya kumhoji mara kadhaa ndani ya kipindi cha wiki mbili. Anashtakiwa kwa makosa ya rushwa na utakatishaji fedha.

Mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam amesema kuwa anakubaliana na uamuzi wa kumfungulia mashtaka Sarkozy na kuahidi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa ushahidi.

Gari lenye mabomu laua 14 karibu na hoteli
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Machi 23, 2018