Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amekataa kuhojiwa mbele ya tume inayomchunguza kuhusu sakata la ufisadi.

Mawakili wa Zuma wamesema kuwa mteja wao ameamua kugoma kwasababu anahisi hatendewi haki wakati wa mahojiano.

“Mteja wetu tangu mwanzo amekuwa akichukuliwa kama mtu mwenye makosa makubwa, sasa anahisi hatendewi haki wakati wa mahojiano,” amesema wakili wa Zuma, Muzi Sikhakhane.

Aidha, Rais huyo wa zamani ametoa maelezo wiki hii katika kile kinachoitwa tume inayotumika na dola kwa maslahi ya watu fulani, ambao Zuma amesema wanalengo la kummaliza kisiasa.

Raymond Zondo, anayeongoza jopo la majaji katika uchunguzi huo, amesema kuwa Tume hiyo haijapewa uwezo wa kuthibitisha kesi dhidi ya mtu yeyote, lakini imepewa uwezo wa kuchunguza na kuhoji juu ya baadhi ya tuhuma.

Zuma amekanusha madai ya ufisadi dhidi yake, akisema alikuwa muhanga wa hujuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake kwa lengo la kummaliza kisiasa, kumvunjia heshima yake na kumuua.

Hata hivyo, Zuma alishinikizwa kujiuzulu katika wadhifa wake wa urais mwaka 2018 na chama tawala cha ANC baada ya kuhusishwa na kashfa mbalimbali za ufisadi, ambapo waemdesha mashtaka wanamtuhumu kuwa ametumia dola za Marekani milioni 20 za mfuko wa umma kuboresha makazi yake binafsi.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 20, 2019
Marekani yatamba kutungua ndege ya kivita ya Iran