Kiungo  wa Simba, Said Ndemla, sasa anajiandaa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuwepo Msimbazi huku ikielezwa lile dili la kwenda kucheza Ulaya limeyeyuka.

Ndemla ambaye mkataba wake wa sasa na Simba unamalizika Aprili, mwaka huu, mwishoni mwa mwaka jana alikwenda Sweden kufanya majaribio kwenye timu ya AFC Eskelistuna na kufuzu.

Hata hivyo, licha ya kufuzu majaribio hayo, Ndemla ameshindwa kujiunga na timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, uongozi umeridhishwa na kiwango cha Ndemla, hivyo wameona bora waendelee kuwa naye ili kukiongezea nguvu kikosi katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

“Mkataba wake unaelekea ukingoni lakini wakati wowote anaweza kuongezewa kwa sababu uongozi unaridhishwa na kiwango chake ukizingatia kwamba tuna michuano ya kimataifa.

“Hii inamaanisha kuwa, huu si wakati wa kuacha wachezaji kama yeye,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo kuzungumzia mustakabali wa Ndemla, alisema: “Lile dili lake kule Sweden tumewaachia Simba waamue kwani bado ni mchezaji wao, vyovyote watakavyosema ni sawa hakuna shida.”

Wakati hayo yakijiri, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amemuahidi kiungo huyo kumpatia gari kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha msimu huu

Chanzo: CHAMPIONI JUMAMOSI

Kunguni watikisa ndege za Uingereza, Ghana yaonya kuzifungia
Waziri Mwakyembe atembelea Serengeti Boys