Mwenyekiti wa Chama Cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe ameripoti katika kituo cha polisi cha Osterbay jijini Dar es Salaam mapema leo asubuhi, kufuatia wito wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mussa Taibu.

Jana, Augene Kabendera aliyezungumza kwa niaba ya Sekretarieti ya Ushirikiano wa Vyama Nane vya Upinzani, alieleza kuwa Jeshi la Polisi liliwasilisha wito katika Ofisi za Chaumma jijini humo unaomtaka Rungwe kuripoti kituoni leo, Juni 4.

Rungwe alikuwa mmoja kati ya viongozi walioshiriki katika kufanikisha azimio la vyama hivyo nane vya upinzani kutangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi wa marudio wa udiwani katika kata 32, kwa madai kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inawatumia Wakurugenzi wa Halmashauri kama wasimamizi wa uchaguzi kinyume na hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa hivi karibuni.

Vyama hivyo nane ni pamoja na ACT-Wazalendo, Chadema, Chaumma, CCK, NCCR-Mageuzi, DP, NLP na UPDP.

Vyama hivyo vinadai kuwa hukumu ya Mahakama Kuu katika kesi namba 6 ya mwaka 2018 iliyofunguliwa na Bob Wangwe akisaidiwa na Wakili, Fatuma Karume ilikataza matumizi ya wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwani wakurugenzi hao ni makada wa chama cha siasa.

Wamedai kuwa wamepokea barua za kushiriki uchaguzi wa marudio katika kata hizo 32 lakini barua hizo zina sahihi ya wakurugenzi wa halmashauri waliosaini kama wasimamizi wa uchaguzi.

Hata hivyo, NEC imekana madai hayo na kueleza kuwa hakuna hukumu yoyote ya Mahakama Kuu iliyokiukwa.

“Hatujafika hatua ya uchaguzi mkuu na vyombo vyote vyenye mamlaka ya nchi havijasita kutekeleza majukumu yake, kwahiyo, hadi hapo tutakapofikia uchaguzi mkuu tutakuwa tunajua sheria zina msimamo gani. Sheria zitakavyokuwa ndivyo zitakavyozingatiwa,” alisema Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.

DC aeleza walivyomnasa mtuhumiwa kiongozi wa Teleza-Kigoma
Video:Ufahamu ugonjwa wa Ini hatari zaidi ya Ukimwi, hauna tiba, dalili, maambukizi