Mshambuliaji kutoka nchini Brazil, Ronaldinho Gaucho amelazimika kuwaomba radhi mashabiki wa klabu yake mpya ya Fluminense, baada ya kuchelewa uwanjani kwa lengo la kutambulishwa mbele yao.

Uongozi wa klabu ya Fluminense ulikuwa umejipanga kumtambulisha Ronaldinho kwa mashabiki kabla ya mtanange wa ligi ya nchini Brazil ambao ulishudia kikosi cha klabu hiyo kikimenyana na Vasco da Gama mwishoni mwa juma lililopita.

Gaucho amesema halikuwa kusudio lake kuchelewa uwanjani hapo na anatambua mashabikli wengi walikuwa na hamu ya kumuona kama ratiba ilivyokua inawaelekeza, lakini haikuwa hivyo, kutokana na sababu ambazo zilikua nje ya uwezo wake ambapo hata hivyo hakuzitaja.

Gaucho mwenye umri wa miaka 35, amesema ni wakati mzuri kwake kuitumikia klabu ya nyumbani kwao Brazil, baada ya kucheza soka nchini Mexico msimu uliopita kwenye klabu ya Queretaro.

Amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo kufanya kazi ipasavyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzake uwanjani, ili kutimiza wajibu wa kutwaa mataji pamoja na kupata matokeo mazuri kila kukicha.

Gaucho alilazimika kutambulishwa kwa mashabiki, wakati wa mapumziko, ambapo hata hivyo mashabiki walionyesha furaha dhidi yake kwa kumlaki kwa kelele na bashasha.

Hatua ya kukubali kujiunga na klabu ya Fluminense, inadhihirisha wazi Gaucho ameikataa ofa ya klabu ya Antalyaspor ya nchini Uturuki ambayo tayari imeshamsajili mshambuliaji kutoka nchini Cameroon, Samuel Eto’o.