Rais wa Marekani, Donald Trump amesema atatumia jeshi kuzima maandamano yanayoendelea nchini humo, endapo viongozi wa majimbo watashindwa kutumia polisi kulinda mali na maisha ya watu wao kwa kutuliza vurugu za waandamanaji.

Maandamano yanaendelea nchini humo kufuatia tukio la askari polisi kumuua George Floyd kwa kumkandamiza na goti shingoni kwa muda mrefu.

Waandamanaji walifika mbele ya jengo la Ikulu ya Marekani, wakishinikiza hatua zichukuliwe huku wakipinga ubaguzi wa rangi ambao wanaamini unafanywa na polisi. Floyd ni Mmarekani Mweusi na aliuawa na askari mzungu.

“Kama majiji au majimbo yatashindwa kuchukua hatua muhimu za kulinda mali na wakaazi wa maeneo yao, mimi nitatoa amri ya kuingiza Jeshi la Marekani kutatua hili tatizo haraka kwa ajili yao,” alisema Trump.

Kwa mujibu wa CNN, helikopta za polisi zilizorusha mabomu ya machozi pamoja na vikosi vya jeshi la polisi vinavyowatawanya waandamanaji vimeendelea na kazi yao, ingawa maandamano nayo bado yanaendelea.

Katika hatua nyingine, pamoja na maelezo ya Trump, kuna baadhi ya matukio yanayowaonesha polisi wakiungana na waandamanaji, kuwakumbatia na hata kupiga magoti na kusali pamoja wakimuombea George Floyd.

Huko Atlanta, Georgia, polisi waliopanga msitari wakiwa na silaha za kuzima vurugu, walipiga magoti mbele ya waandamanaji na kusali pamoja.

Taswira nyingine imewaonesha polisi walioziba sura zao kwa vifaa vyenye gesi ya kuwasaidia kupumua na kofia ngumu wakimkumbatia mwandamanaji, katika siku ya nne ya maandamano hayo.

Jijini New York, Mkuu wa Idara ya Polisi ya jiji hilo, Terence Monahan alionekana pia akimkumbatia mwandamanaji, wakati wakiendelea na juhudi za kurejesha amani.

Trump ameeleza kuwa yeye ni mshiriki wa waandamanaji wote wanaoandamana kwa amani, na pia ni Rais wa sheria na amri.

Baada ya kueleza hayo, alienda kwenye jengo la kanisa la St. John’s Episcopal, kanisa ambalo marais wa Marekani wamekuwa wakilitumia kufanya ibada kwa zaidi ya miaka mia moja sasa. Sehemu ya kanisa hilo ilichomwa na waandamanaji, Jumapili.

Ibrahim Ajibu alimwa mshahara Simba SC
Frank Lampard kuingia vitani