Magwiji wa soka mjini Madrid, Hispania Real Madrid wazidi kufifisha matumaini ya FC Barcelona kutetea ubingwa msimu huu, baada ya kufanikiwa kuchapa Getafe bao moja kwa sifuri.

Katika mchezo huo ulioonekana kuwa mgumu na kusababisha kipindi cha kwanza kuisha kwa sare ya bila kufungana, Real Madrid walipata bao mnamo dakika ya 79 kupitia mkwaju wa penati uliopigwa na nahodha na beki wao hodari Sergio Ramos.

Mpaka filimbi ya mwisho inapulizwa kuashiria kuisha kwa mchezo huo, Real Madrid walitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Matokeo hayo yanaifanya Real Madrid kufikisha alama 74 na kuacha nafasi ya alama nne dhidi ya mpinzani wake Barca, ambaye anashika nafasi ya pili akiwa na alama 70, huku wote wakiwa wamecheza michezo 33.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane alizungumza na vyombo vya habari, na kusema kuwa bado mapambano yanaendelea.

” Tumeshinda lakini siwezi kusema chochote, bado tuna michezo mitano inayofuata, kwangu ni kama hatujashinda kitu, ingawa zilikuwa ni pointi tatu muhimu, bado tunahitaji kuendelea kupambana zaidi, tuna furaha juu ya umoja wetu katika timu, na hilo ndio jambo zuri kwetu.” Alisema

Watu 55,000 wakutwa na virusi vya corona ndani ya siku moja Marekani
Nugaz: Sisi hatufungwi