Meneja wa mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa barani Ulaya Real Madrid  Santiago Solari, ana matumaini makubwa ya kukiona kikosi chake kikirejea katika njia ya ushindi, baada ya kupoteza mchezo wa ligi ya Hispania mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa na Eibar mabao matatu kwa sifuri.

Solari anatumaini hivyo baada ya kushuhudia nahodha na beki wake Sergio Ramos akitoa lawana za wazi dhidi ya wachezaji wenzake, mara baada ya mchezo huo wa ligi ya Hispania, ambao uliwastajaabisha wengi kutokana na mwanzo mzuri wa muagentina huyo, ambaye alichukua nafasi ya Julen Lopetegui, majuma kadhaa yaliyopita.

Kikosi cha Real Madrid leo kinarejea katika majukumu ya kusaka alama tatu muhimu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwa kuwakabili wababe wa mji wa Roma- Italia (AS Roma) ambao watakua nyumbani Stadio Olimpico.

Solari ameongea katika mkutano na waandishi wa habari na kusema: “Kitendo cha kufungwa na Eibar mwishoni mwa juma lililopita, ni fundisho kubwa kwa kila anaehusiaka na klabu hii, tumejifunza mengi kupitia mchezo huo, tunaamini kwenye mchezo wetu dhidi ya AS Roma kutakua na mabadiliko makubwa ya kiuchezezaji.”

“Real Madrid Inapita katika kipindi kigumu, hatuna budi kuafikiana na changamoto hiyo, lakini jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunaendelea kupambana na kupata matokeo mazuri.”

Hata hivyo Solari alikataa kuzungumzia suala la beki na nahodha wake Ramos, la kuwatupia lawama wachezjai wenzake mara baada ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Eibar.

Kwa upande wa wenyeji AS Roma nao watahitaji kurekebisha makosa yaliyopelekea kupoteza mchezo wao wa ligi ya Serie A wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Udinese, kwa kuhakikisha wanaifunga Real Madrid.

Hata hivyo kikosi cha meneja kutoka nchini Ureno Di Francesco kitawakosa Lorenzo Pellegrini na Robin Olsen ambao ni majeruhi.

Kabla ya kuumia kwa wawili hao AS Roma tayari ilikua na majeruhi wengine kama kiungo na nahodha Daniele De Rossi, Diego Perotti na Javier Pastore, lakini wamepata taarifa njema za kurejea kwa beki Kostas Manolas, ambaye anatarajiwa kucheza leo usiku.

Katika mchezo wa kwanza wa kundi G, Real Madrid walifanikiwa kuchomoza ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya AS Roma kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid.

RC Mndeme afuta likizo za watumishi
Bruno Genesio aihofia Manchester City

Comments

comments