Serikali Mkoani Kagera imeawataka wananchi ambao wamejipanga kujihusisha na vitendo vya kuhujumu zao la kahawa kwa kuanza biashara ya magendo wakiwa na lengo la kuwatapeli wakulima kuacha mara moja.
 
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa huo, Jenerali Marco Gaguti Wilayani Karagwe kwenye Mkutano Mkuu wa 32 wa KDCU LTD ambapo amesema kuwa tayari ameanza kusikia fununu za baadhi ya watu kutaka kukigawa chama cha KDCU LTD katika vyama viwili ambavyo vitawakilisha Wilaya za Karagwe na Kyerwa na kuonya kuwa jambo hilo haliwezi kutokea na halitakiwi kufikiriwa wala kujadiliwa.
 
“Kama kuna mwananchi, kundi la watu, baadhi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika au kiongozi yeyote ana wazo la kukigawa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Karagwe na Kyerwa Development Co-operative Union Limited (KDCU LTD) ahame mara moja Mkoa wa Kagera au akafanye hivyo nje ya mkoa huu lakini sipo tayari kuona jambo hilo linatokea.” amesema Gaguti
 
Aidha, amesisitiza kuwa kwasasa anatamani Mkoa wa Kagera ungekuwa na Chama Kikuu cha Ushirika kimoja chenye nguvu na kuwahudumia wakulima lakini si kuwa na Vyama vya Ushirika vingi ambavyo vitauingiza mkoa katika migogoro na haviwezi kuwasaidia wakulima kuendeleza kilimo cha kahawa.
 
Kwa upande wake Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate akiongea na wajumbe wa mkutano huo amewaonya viongozi wa KDCU LTD kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa fedha za wakulima katika Vyama vya Msingi vya chama kikuu hicho ambapo amesema kuwa kwa utafiti wake wa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wamehujumu au kutumia vibaya fedha za wakulima katika maeneo yao.
 
Hata hivyo, Mkoa wa Kagera umekusanya na kuuza jumla ya kilo milioni 58.9 za Kahawa na Chama Kikuu cha KDCU LTD kimekusanya asilimia 67% kahawa zote. Chama cha KDCU LTD kilikuwa kimepanga kukusanya tani elfu 40 na kufanikiwa kukusanya tani elfu 39 sawa na asilimia 98% na tayari chama hicho kimepata faida ya shilingi milioni 260.
CCM Njombe yasema Ushindi ni lazima
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 6, 2019

Comments

comments