Mkuu wa Mkoa (RC) wa Shinyanga, Zainab Tellack amesema kuwa lengo la kukusanya kadi za ATM za watumishi wa umma hususan katika wilaya ya Kishapu ni pamoja na kulinda maslahi yao.

RC Tellack amesema Serikali ya mkoa huo imebaini kuwa watumishi wengi wa umma katika Wilaya ya Kishapu wamesalimisha kadi zao za ATM kwa watu binafsi waliowakopesha, hali inayosababisha wengi wao kukatwa mshahara wote ili kulipia madeni, kinyume na sheria.

Mkuu huyo wa mkoa amesema wamelazimika kuingilia suala hilo ili kufanya udhibiti kwa kuzingatia maslahi ya wakopeshaji pamoja na watumishi wa umma.

“Wote tunajua sheria. Sio nia ya Serikali kuwafanya waliowakopesha kupata hasara… La Hasha! Tunataka kulinda haki na maslahi ya pande zote kwa mujibu wa sheria, ndio maana mwezi huu tumeruhusu hata watumishi ambao hawajaitikia agizo la uhakiki wa ATM zao kulipwa mishahara yao,” alisema RC Tellack.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kishapu, Mang’era Mang’era alitoa tangazo linalowataka watumishi wote wa umma kuwasilisha ofisini kwake kadi za ATM kwa ajili ya uhakiki. Tangazo hilo lilitaja Mei 23, 2019 kuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha kadi hizo.

“Kutokufika kwenye zoezi hili, mshahara wako utazuiwa,” inasomeka sehemu ya tangazo la Mkurungezi Mtendaji wa Kishapu.

Akizungumzia uamuzi huo, Mang’era alisema kuwa lengo ni kuwasaidia watumishi na kufahamu idadi ya watumishi ambao wametoa kadi zao za ATM kwa wakopeshaji.

“Kiutaratibu mtumishi akikopa benki au taasisi yoyote ya fedha, anatakiwa kubakiza angalau moja ya tatu ya mshahara wake baada ya marejesho kwa ajili ya mahitaji yake binafsi na familia. Lakini baadhi hawazingatii masharti haya,” Mang’ere anakaririwa na Mwananchi.

Alisema hali hiyo inawafanya watumishi kukopea mshahara wote na mwisho kukosa kabisa mshahara. Aliongeza kuwa hali inasababisha kushindwa kumudu gharama za maisha kwa ajili yao na familia zao.

Serikali ya mkoa huo pia imesema inataka kudhibiti viwango vya juu vya riba zinazotolewa na wakopeshaji ambao wengine hufikia asilimia 50.

LIVE: Rais Magufuli akiwa Afrika Kusini, apokelewa kwa shangwe
Umoja wa Ulaya watoa tamko baada ya May kujiuzulu