Rapa wa Marekani XXXTentacion ambaye alipanda kwa kasi na kukaa kwenye kilele cha chati za muziki wa rap ndani ya miezi sita kwa albam zake mbili, ameuawa kwa kupigwa risasi na mtu ambaye bado hajajulikana.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi la Broward, rapa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 20 alipigwa risasi jana (Jumatatu) majira ya saa kumi jioni kwa saa za eneo hilo, alipokuwa akitembea Kusini mwa Florida.

Rapa huyo ambaye pia alikuwa mwimbaji, jina lake halisi likiwa ni Jahseh Onfroy, alikimbizwa hospitalini baada ya kupigwa risasi lakini alipoteza maisha akiwa hospitalini.

XXXTentacion alikuwa anakabiliwa na kesi ya kumshambulia mpenzi wake wa zamani akiwa mjamzito pamoja na matukio mengine tata.

Albam yake ya kwanza, ‘17’ iliyotoka Disemba mwaka jana ilishika nafasi ya pili kwenye chati za Billboard 200 na Machi mwaka huu albam yake ‘?’ ilishika nafasi ya kwanza kwenye chati.

Kendrick Lamar alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono kazi za rapa huyu mdogo aliyekuwa na mamilioni ya wafuasi kwenye mitandao ya kijamii, ingawa mara kadhaa mashabiki walikuwa wakiwashindanisha kutaka kujua nani mwenye uwezo zaidi.

Mitandao ya kijamii imegubikwa na jumbe za majonzi kutoka kwa watu maarufu na mashabiki wake.

Mali za mpinzani wa Kagame zapigwa mnada nchini Rwanda
Habari kubwa katika magazeti ya leo Juni 19, 2018