Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi mabalozi watatu waliomaliza muda wao wa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini Tanzania wawaeleze watakaokuja kuchukua nafasi hizo kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo na Tanzania.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Julai 11, 2018 wakati akiwaaga mabalozi hao ambao ni Hawa Olga Ndilowe – Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Mhe. Katarina Rangnitt – Balozi wa Sweden nchini Tanzania pamoja na Mhe. Hanne-Marie Kaarstad  Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuwashukuru kwa kazi nzuri walizozifanya katika kipindi walichoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

“Natambua mchango mkubwa ambao nchi hizo zinautoa kwa maendeleo ya Tanzania, na niwasihi muwaeleze Mabalozi watakaokuja kuchukua nafasi zenu kuendeleza ushirikiano  mzuri uliopo kati ya nchi hizo na Tanzania na dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha uhusiano huo unakuzwa kwa kujikita zaidi katika diplomasia ya uchumi”,amesema Dkt. Magufuli.

Kwa upande wao Mabalozi hao kwa pamoja wamempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizozifanya katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kusimamia rasilimali za Taifa, kutekeleza miradi mikubwa ya kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji kupitia mwongozo wa uwekezaji ‘blue print’ ambao umelenga kuondoa kero zinazowakabili wawekezaji.

Kwa upande mwingine, Mabalozi hao wamemuahidi Rais Magufuli kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kuinadi Tanzania katika nchi zao ili kukuza uwekezaji, biashara, utalii na ushirikiano utakaokuwa chachu ya manufaa kwa Tanzania na nchi hizo.

Everton, FC Barcelona wamjadili Yerry Mina
Manuel Pellgerini asajili jembe la Ukraine