Rais John Magufuli ameeleza sababu za kumteua Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo akimkumbusha machachali yake akiwa bungeni.

Akizungumza muda mfupi baada ya kumuapisha, Rais Magufuli alisema alikuwa akimsikiliza Bashe akitoa michango mizuri yenye uchambuzi wa takwimu bungeni. Hivyo, anampa mtihani wa kuiweka kwenye vitendo.

“Nimekuwa nakusikiliza sana Bungeni, michango yako imekuwa ni mizuri. Unatoa analysis (uchambuzi) ya namna kilimo kinavyoweza kuleta production (uzalishaji) katika uchumi wa nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

“Uchambuzi ule umenivutia na nilipenda. Sasa zile zilikuwa za bungeni, nataka sasa ukaziweke kwenye practical (vitendo). Na ndio maana nimekuweka kwenye wizara ya kilimo, hayo yote ya theory (nadharia) uliyokuwa ukiyazungumza bungeni na tukafurahia sasa yakawe kwenye vitendo na ukayatekeleze kwelikweli,” aliongeza.

Aidha, Rais Magufuli alieleza kuwa ana imani na Mbunge huyo wa Nzega na kwamba anaamini haitakuwa vigumu kwake kubadili nadharia kuwa vitendo.

Naye Bashe, alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Naibu Waziri na kuahidi kufanya kazi kwa bidii. Alitumia sentesi anayopenda kuitumia Rais Magufuli kutoa ahadi, “sitakuangusha.”

“Niliyokuwa nayasoma kwenye makaratasi na taarifa bungeni sasa naenda kujionea na kujifunza na kuyafanya kwa vitendo,” alisema Bashe.

Bashe anachukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Waziri wa fedha Kenya amajisalimisha polisi kwa tuhuma za Ufisadi
JPM aeleza sababu za kumng’oa Makamba, Simbachawene akandamizia