Jeshi la Polisi nchini Kenya linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kujipatia fedha wakijifanya ni viongozi wa ngazi za juu Serikalini, na mmoja wao kujifanya kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, watu hao ambao wanaishi maisha ya kifahari wamekuwa wakiwapigia simu matajiri nchini humo, mmoja akiwa anaigiza vyema sauti ya Rais Kenyatta na kuwataka kutoa fedha kwa sababau mbalimbali za uongo.

Mmoja wa matajiri walioathirika na Rais feki wa Kenya ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Sameer Africa anayefahamika kwa jina la Naushad Merali ambaye alipokea simu na akajikuta akitoa kiasi kikubwa cha fedha.

Bado kiwango halisi cha fedha hakijafahamika rasmi lakini Daily News imeripoti kuwa Merali alitapeliwa Sh10 milioni za Kenya.

Watu hao waliofikishwa jana mahakamani ingawa hawajafunguliwa kesi rasmi ni Joseph Waswa, Duncan Muchai, Isaac Wajekeche, William Simiyu, David Luganya, Gilbert Kirunja na Anthony Wafula.

Watuhumiwa kesi ya kutumia sauti ya Rais Uhuru Kenyatta, viongozi wa Serikali kutapeli

Polisi wameeleza kuwa hawajawafungulia kesi rasmi kwakuwa upelelezi bado unaendelea na suala hilo lina mambo mengi.

“Kutokana na ugumu wa kupeleleza na idadi ya watuhumiwa katika suala hili, inatarajiwa kuwa upelelezi utahusisha kupitia nyaraka nyingi sana ikiwa ni pamoja na hati za malipo za benki na upembuzi wa mawasiliano ya simu,” Daily News imekariri ripoti ya Polisi.

Watu hao wanadaiwa kuwa na ukaribu na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa ofisi kubwa za Serikali ambao huwasaidia kukamilisha baadhi ya taratibu zao ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka na kuwapa ofisi watumie kwa muda.

“Ili kukamilisha mipango yao na wazabuni wanaowaibia, watu hao kwa kushirikiana na maafisa wa Serikali wasio waaminifu pamoja na askari polisi, walikuwa wakighushi nyaraka zenye nembo halisi za Serikali na kuwaalika watu hao kwenye ofisi kubwa za Serikali kwa lengo la kuwasainisha nyaraka feki,” tovuti ya The Star imeripoti kuhusu taarifa ya jeshi la polisi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ameeleza kuwa Merali ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Sameer Group hakuweza kutoa maelezo yake kwakuwa yuko nje ya nchi, lakini msaidizi wa tajiri huyo aliyemtaja kwa jina moja la Gitonga aliandikisha maelezo yake kuhusu suala hilo.

NMB yatumia zaidi ya bil.1 kusaidia mashule
Asherehekea mwanaye kufungwa jela miaka 30, Mtwara