Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema kuwa amewaagiza polisi na jeshi kutomuonea huruma mtu yeyote anayejaribu kuvuruga uchaguzi wa rais nchini humo ambao umeahirishwa hadi Jumamosi wiki hii.

Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) ilitangaza Ijumaa jioni masaa kadhaa kabla ya vituo vya kupiga kura kufunguliwa kwa wapiga kura milioni 84 waliosajiliwa katika daftari ya kupiga kura na kutangazwa kwamba uchaguzi utaahirishwa kwa wiki moja.

INEC imesema kuwa uchaguzi wa rais na wabunge utafanyika Jumamosi, wakati uchaguzi wa magavana na baraza la wawakilishi utasogezwa mbele hadi machi 9 mwaka huu.

Aidha, Buhari mwenye umri wa miaka 76, akizungumza katika mkutano wa dharura wa chama chake cha All Progressives Congress (APC) ameituhumu INEC kuwa haina uwezo na kumuonya yeyote atayejaribu kuharibu masanduku ya kupigia kura na vifaa vya uchaguzi.

“Yeyote anayefikiria anaushawishi katika eneo lake kuongoza kikundi cha wahuni au kuiba masanduku au kuvuruga mfumo wa uchaguzi, atafanya hivyo kwa kulipa thamani ya maisha yake,”amesema Buhari.

Hata hivyo, Chama cha APC na chama cha upinzani cha People’s Democratic Party vimekuwa vikituhumiana kwa jaribio la kutaka kuiba kura, lakini rais Buhari anakabiliwa na changamoto nzito kutoka mgombea wa chama cha upinzani PDP, Atiku Abubakar ambaye alikuwa makamu wa rais wa zamani.

B12 afunguka kinachokosekana sasa kwenye Hip-Hop, Rap Bongo
Video: Prof Lipumba apata pigo la kwanza CUF, DCI afunguka shambulio la Tundu Lissu