Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa, Simba ina nafasi kubwa ya kuifunga TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wao wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Simba inatarajia kuvaana na Mazembe Aprili 5, mwaka huu katika mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika ambapo wataanzia nyumbani kisha kumalizia ugenini Aprili 12.

Simba ilifanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuichakaza AS Vita kwa idadi ya mabao 2-1, hivyo inahitaji kujipanga ili kushinda katika mchezo wake huo.

“TP Mazembe ya sasa siyo ile ya zamani, kwa sasa haipo vizuri japo si sana, ukiangalia kwenye msimamo wa ligi yao ipo nafasi ya pili ikiwa imecheza mechi 25 na pointi 58 huku Vita ambao tumewafunga wakiwa wanaongoza ligi wakiwa na pointi 62 wakiwa wamecheza michezo 25, na ukiangalia mchezo wao wa mwisho walivyokutana, Vita iliifunga TP Mazembe mabao 3-0 na sisi tumewatoa Vita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, hivyo unaweza kuona jinsi hali ilivyo, Simba ni timu nzuri na ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kuifunga Mazembe,”amesema Rage

Hata hivyo, Rage amewataka wachezaji kutobweteka na badala yake wapambane hadi tone la mwisho ili waweze kufanikiwa kushinda katika mchezo huo, ambapo amesema TP Mazembe ya sasa siyo ile ya zamani, kwani kwasasa haina sapoti kubwa kama ilivyokuwa huko nyuma kwa kuwa rais wao, Moise Katumbi hayupo DR Congo.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 25, 2019
Video: ACT- Wazalendo, Chadema vita mpya, CUF yapukutika Zanzibar