Beki wa pembeni kutoka nchini Brazil, Rafael Pereira da Silva, amefichua siri ya kuondoka kwake kwenye klabu ya Man Utd, ambayo ilimsajili mwaka 2008 wakati wa utawala wa Sir Alex Ferguson.

Rafael, ambaye kwa sasa ni mchezaji halali wa klabu ya Olympic Lyon ya nchini Ufaransa, amesema alianza kuona dalili ya kuondoka Old Trafford mara baada ya kustaafu kwa babu Ferguson aliyekua amemuamini kwa kiasi kikubwa tangu alipomsajili akitokea nchini kwao Brazil kwenye kituo cha kulea na kuendeleza vipaji kwa vijana cha klabu ya Fluminense.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 25, amesema mipango ya mameneja waliokuja baada ya babu huyo kuondoka ilikua inadhihirisha hakuwa na muda mrefu wa kuendelea kuitumikia klabu ya Man Utd, ambayo amekiri alikua akiipenda na kuithamini.

Hata hivyo Rafael, ameonyesha kuchukizwa sana na mwenendo wa meneja wa sasa wa Man Utd, Louis van Gaal kwa kusema alimuonyesha dhahir hamuhitaji kutokana na kushindwa kumtumia mara kwa mara msimu uliopita.

Rafael, akaenda mbali zaidi kwa kubainisha kwamba aliwahi kuambiwa na mtu wake wa karibu ambaye hakua tayari kumuweka wazi, Van Gaal amekua na kasumba ya kutowakubali wachezaji kutoka nchini Brazil, hivyo kuajiriwa kwa meneja huyo kutoka nchini Uholanzi pale Old Trafford alitambua hakuwa na maisha marefu zaidi.

Amesema dalili zilianza kuonekana tangu siku ya kwanza walipoanza kufanya nae kazi na dhahiri Van gaal alionyesha kumchukia huku akisisitiza tabia hiyo haikukoma hadi alipofanya maamuzi ya kumuuza majuma kadhaa yaliyopita.

Pamoja na kutoboa siri hiyo, Rafael ameitakia Man Utd, kila la kheri msimu huu ili iweze kufikia lengo la kurejesha heshima yake iliyopotea tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson.

Tomas Rosicky Anastahili Kisu
Wananchi Waandamana Kupinga Goli La Mkono Kwa Nape