Mfalme wa RnB, R Kelly ameendelea kusota ndani ya selo za polisi baada ya kushindwa kutoa $100,000 kwa ajili ya kujidhamini, kutokana na tuhuma za kuwanyanyasa kingono wanawake wakiwemo wasichana wadogo.

Jaji wa Chicago alimpa nafasi R Kelly kujidhamini kwa $1 milioni Jumamosi iliyopita, kutokana na mashtaka kumi yalikuwa yanamkabili yakihusisha wanawake wanne ambao kati yao watatu wanadaiwa kuwa walikuwa wasichana wadogo. Hivyo, ilikuwa $250,000 kwa kila muathirika.

Lakini ili kufanikiwa kuondoka ndani ya selo za polisi, alipaswa kutoa 10% ya kiwango cha dhamana yake, ambacho ni $100,000.

Ingawa mwanasheria wake, Steve Greenberg alisema kuwa amefurahishwa na kiwango cha dhamana kilichotajwa kulinganisha na tuhuma zinazomkabili mteja wake, alidai kuwa mteja wake huyo hivi sasa hana fedha.

Greenberg alidai kuwa R Kelly hana pesa hizo kwenye akaunti za benki kutokana na kuwa na matumizi mabaya ya fedha na usimamizi usiokuwa bora.

Alisema kuwa mteja wake atajitahidi kukusanya kiwango hicho cha fedha angalau kinachoweza kumsaidia kutoka ndani ya selo za polisi. Hata hivyo, hadi jana jioni alishindwa kufanikisha hilo.

R Kelly alishikiliwa na polisi wiki iliyopita baada ya kusakamwa na tuhuma za udhalilishaji wa kingono wa wanawake kadhaa ikiwa ni pamoja na wasichana wadogo. Makala ya ‘Surviving R Kelly’ ndiyo iliyoongeza nguvu zaidi ya kusakamwa na mwisho ameingia kwenye shida kubwa ya mkono wa sheria.

Wabunge wanne kuhojiwa kuhusu sakata la video ya ngono
Majaliwa: Rais Magufuli anataka watanzania wote wapate huduma za afya karibu na makazi yao